Na Said Mwishehe, Michuzi TV
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Chama hicho pamoja na Serikali zake zinatambua na kuheshimu vyombo vya habari pamoja na wanahabari hasa kwa kutambua tasnia hiyo ina mchango mkubwa wa maendeleo ya Taifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Shaka Hamdu Shaka kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Mei 4,2021 amesema kila ifikapo Mei 4 ya kila mwaka Dunia huadhimisha siku ya Habari, hivyo CCM na Serikali zake zinatambua na kuheshimu vyombo vya habari.
"Serikali yoyote duniani, vyama vya siasa, vyama vya kijamii, NGOS na mashirika hiari ya kijamii na mashirika ya dini ili yafikie malengo yake kisera, hutegemea kupata msukumo wa nguvu za kitaaluma na kuungwa mkono na Vyombo vya Habari .
"Tasnia ya Habari inapokuwa huru na waandishi wakiandika kwa uwazi, uhalisia na ukweli na kutumia kalamu zao kwa weledi na maadili husaidia kuharakisha maendeleo. Ni vigumu kwa sekta ya umma au sekta ninafsi kutimiza shabaha zake unapokosekana Uhuru wa Habari.
"Pamoja na uhuru wao, vyombo vya habari na waandishi wanatakiwa kuzingatia na kuheshimu sheria za nchi, kufuata maadili, miiko na kanuni za taaluma ya uandishi wa habari unaojenga nchi badala ya kalamu zao kupotosha au kuchochea mifarakano,"amesema Shaka.
Amefafanua CCM kama ilivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi (2020 – 2025) Sura ya 06, Fungu la 125, kitaendelea kuzielekeza Serikali zake kuheshimu tasnia ya habari huku wakiwahimiza waandishi wa habari kuandika habari zitakazojenga nchi badala ya zile za kulibomoa Taifa
"Chama kitahakikisha uhuru wa vyombo vya habari unaimarishwa na kulindwa, na kwamba wamiliki na wanahabari wanazingatia maadili na weledi katika kazi zao. Chama kinafurahi pale waandishi wa habari wanapoandika kwa kuzingatia weledi katika tasnia yao baada ya kupata habari kutoka vyanzo ama mamlaka husika na si habari za kuifarakanisha jamii,"amesisitiza.
Aidha amesema CCM inavikumbusha vyombo vya habari kutambua vina haki na wajibu wa mashambani na Wafanyakazi viwandani na kwamba kalamu zao zisiache kuandika ukweli kuhusu maendeleo ya kilimo, mifugo, madini, uwekezaji, afya na jamii ya Watanzania, lakini vikosoe na kurekebisha kama kuna haja ya kufanya hivyo.
Pia vyombo vya habari viendelee kufichua na kupiga vita vitendo vya ufisadi, vikemee ubadhirifu wa mali za umma, wizi na kushamirisha mapambano dhidi ya adui rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa Umma.
Shaka amesema Chama hicho kitafanya kila linalowezekana kuimarisha vyombo vya habari vya Chama ili vifikishe habari za kisera na kimaendeleo kwa haraka na kwa uhakika katika jamii. Vyombo vya habari na waandishi wa habari wana kazi na wajibu wa kueleimisha, kufundisha na kuburudisha jamii. "Kwa muktadha huo CCM inawataka wanahabari kutimiza majukumu ya kufichua badala ya kuficha ukweli kwa kuzingatia maadili na miiko ya kisheria iliyopo".
Ameongeza kuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza angependa kusikia habari za kweli zikiwafikia Wananchi kwa haraka mahali popote walipo mijini au vijijini.
"Ndiyo maana hivi karibuni aliielekeza Serikali kuzifungulia TV za mitandaoni na kuwataka wamiliki na wahariri wao kufuata Sheria, kuheshimu maadili ya uandishi wa habari na kuzingatia Kanuni zake, kama ilivyosisitizwa katika Ilani ya Uchauzi ya CCM,"amesema.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment