Na Ramadhani Ali – Maelezo
Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright ameahidi Serikali ya nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha afya za wananchi.
Ameeleza kuridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa katika mapambano dhidi ya maradhi ya Maleria na kusema kuwa Marekani itaendeleza mkakati utakaohakikisha maradhi hayo yanamalizika kabisa.
Balozi Donald ameeleza hayo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui Ofisini kwake Mnazimmoja.
Balozi wa Marekani amemueleza Waziri wa Afya kuwa Serikali ya nchi yake imetenga fedha maalumu kwa ajili ya kupambana na maradhi ya Ukimwi nchini Tanzania.
Ameahidi kuwa nchi hiyo ipo tayari kusaidia masuala ya chanjo ya Covid 19 ili Zanzibar iendelee kuwa salama na maradhi hayo ambayo yamekuwa tatizo kubwa katika nchi nyingi duniani.
Aidha Balozi Donald ameeleza suala la Wafanyabiashara wa Marekani kuja kuwekeza vitega uchumi Zanzibar ili kuwapatia vijana wengi ajira na kuimarisha uchumi wan chi.
Amesema vijana ndio nguvu kazi ya nchi na iwapo watapatiwa ajira za uhakika wataweza kusaidia maendeleo ya nchi yao kwa kiwango kikubwa na kuipunguzia Serikali gharama zisizokuwa na ulazima.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui amemueleza Balozi Donald kuwa maradhi ya Maleria yapo kwa asilimia moja hivi sasa na Wizara ya Afya huchukuwa hatua za dharura sehemu ambayo atapatikana mgonjwa wa maradhi hayo.
Akizungumzia maradhi ya Covid 19 Waziri Mazurui amesema kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa Zanzibar hajapatikana mgonjwa wa maradhi hayo na tahadhari kubwa inaendelea kuchukuliwa kwa wenyeji na wageni wanaoingia nchini.
Amesema Zanzibar haijaweka vizuizi kwa watu kuingia na kutoka lakini milango mikuu yote ya kuingilia kumewekwa mashine maalumu za kufanyia uchunguzi ili kuhakikisha maradhi hayo hayaingia nchini.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright alipofika Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Zanzibar. Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright akiagana na Waziri Nassor Mazrui baada ya mazungumzo yao yaliofanyika Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Mnazimmoja.Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment