Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ameagiza kuwa, ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha kV 220/33 katika Kituo cha umeme cha Mtera ukamilike kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.
Alitoa agizo hilo tarehe 9 Mei,2021 wakati alipofanya ziara katika kituo cha kufua cha umeme cha Mtera na kukagua sehemu ya Bwala la Maji la Mtera, kazi ya uzalishaji umeme na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kipya cha kupoza umeme ambapo aliambatana na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO.
“Tunapanua kituo cha kupoza umeme kilichopo hapa ili kukiongezea nguvu na hivyo kuweza kusambaza umeme katika Mkoa wa Iringa na Dodoma, kazi ilichelewa kidogo kutokana na masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi, hivyo nimetoa maelekezo kuwa Mkandarasi anatakiwa kufanya kazi usiku na mchana.
”Alisema Wakili Byabato Alieleza kuwa, tayari baadhi ya kazi zimeshafanyika katika kituo hicho kipya cha kupoza umeme ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ufikishaji wa transfoma na vifaa vingine vya umeme vinavyohitajika.
Kuhusu hali ya uzalishaji umeme katika Kituo cha Mtera, alisema kuwa, kituo hicho kinazalisha megawati zote 80 kutoka katika mitambo miwili iliyopo kituoni hapo ambapo kila mtambo unazalisha megawati 40, hivyo aliwapongeza watalaam wa TANESCO kwenye kituo hicho kwa kufanya kazi kwa weledi, kujituma na ubunifu.
Aidha, alisema kuwa, kuna maji ya kutosha kuzalisha umeme katika Bwawa la Mtera, yenye kina cha mita 698.50 na kwamba maji yaliyopo yana uwezo wa kuzalisha umeme katika kipindi cha mwaka mzima hata kama mvua hazitanyesha.
Vilevile alisema kuwa, Serikali inatilia mkazo suala la ujenzi wa miundombinu ya umeme ili kuweza kuwafikishia umeme wananchi wengi zaidi na alitoa rai kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme na kuunganisha umeme mara unapofika kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema kuwa, watamsimamia mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi kituo kipya cha kupoza umeme cha Mtera ili kuhakikisha kuwa kazi husika inakamilika mwezi Septemba kama ambavyo imeagizwa na Naibu Waziri.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati, alikagua kazi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika kijiji cha NhiNhi kilichopo wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma na kumuagiza mkandarasi, kampuni ya A to Z, kupeleka umeme kwenye kijiji hicho kabla ya tarehe 30 Juni mwaka huu, na umeme huo ufike kwenye Taasisi zote za umma ikiwemo Shule na Kituo cha Afya.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa kwanza kutoka kulia) akikagua moja ya transfoma itakayofungwa katika kituo kipya cha kupoza umeme cha Mtera.Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (aliyenyoosha mkono) akitazama moja ya mashine za kuzalisha umeme katika Kituo cha kufua umeme cha Mtera ambayo imewekwa kama spea katika kituo hicho.
Kaimu Mhandisi Mkuu katika Kituo cha kufua umeme cha Mtera, Phesto Chikongoye (kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato kuhusu uendeshaji wa mitambo mbalimbali ya umeme katika kituo hicho.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa kwanza kutoka kulia) akiangalia kiwango cha maji katika Bwawa la Mtera ambayo yanatumika kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 80 katika Kituo cha kufua umeme cha Mtera. Kushoto kwake ni Meneja wa Kituo cha kufua umeme cha Mtera, Elias Mwalukilo
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment