SERIKALI YATETA NA WASHIRIKA WA MAENDELEO JIJI DAR ES SALAAM: WAAHIDI KUCHANGIA MAENDELEO YA NCHI | Tarimo Blog
Na Saidina Msangi na Josephine Majura, Dar es Salaam
Serikali imeeleza kuwa itaendeleza ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa sekta zinazogusa watu wengi nchini ikiwemo sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi zinapewa kipaumbele ili kuwezesha ukuaji wa uchumi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, alipokuwa akifungua mkutano wa Majadiliano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.
Bw. Tutuba alisema kuwa mkutano huo ni wa kwanza tangu Tanzania ilipotangazwa kuingia kwenye uchumi wa kati na kuwashukuru wadau wa maendeleo kutokana na michango yao ambayo wamekuwa wakiitoa iliyoiwezesha Tanzania kupiga hatua hiyo.
“Mchango wa wadau una thamani katika kuiwezesha Tanzania kuingia uchumi wa kati na kuwasihi kuendeleza ushirikiano huo ili nchi iweze kusonga mbele zaidi na kuahidi kuwa Serikali itasimamia vizuri matumizi ya fedha za misaada kwa maendeleo ya taifa”, alisisitiza Bw. Tutuba.
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kufanya kazi kwa kuhakikisha mipango yote iliyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa Awamu ya Pili ambao utaisha muda wake mwaka huu mwezi wa sita inatekelezwa na pia itaendelea kutekeleza mipango iliyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.
Aidha, Bw. Tutuba amewataka washirika wa maendeleo kuiunga mkono Serikali kwenye maeneo yote ya miradi ya vipaumbele na kuwaomba wauchambue Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa na kuangalia maeneo ya kipaumbele watakayoelekeza rasilimali zao ikiwemo fedha na utaalam..
Bw. Tutuba aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni sekta za elimu, afya, maji, sekta ya ukuzaji wa uchumi, miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa miundombinu ya umeme kama Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, miundombinu ya usafirishaji, barabara na kuwasihi wadau wa maendeleo kutoa fedha kwa ajili ya miradi hiyo.
Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini hivyo ni vema kila Mtanzania akajishughulisha kujipatia kipato halali na kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.
Bw. Tutuba alitoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanalipa kodi stahiki ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wadai risiti inayolingana na thamani ya fedha walizolipa kila wanaponunua bidhaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti mwenza wa Wadau wa Maendeleo nchini, ambayenni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchi Tanzania Bw. Zlatan Milisic alisema kuwa mkutano huo umefanyika katika kipindi muafaka ambapo Serikali inaelekea kuanza kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka mitano.
Alieleza kuwa wanathamini juhudi za serikali kuwashirikisha wadau wa maendeleo katika kuandaa mipango ya maendeleo na kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha utekelezaji wake.
Alisema kuwa mkutano huo utawezesha kujua hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara nchini (Blue Print) ambao ni muhimu katika kuiwezesha Tanzania kupata maendeleo endelevu na kufikia malengo yake ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa kuboresha ufanyaji biashara nchini.
Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha wataalamu kutoka Serikalini na Washirika wa Maendeleo kutoka ofisi za balozi mbalimbali nchini. Mkutano mwingine unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba ambapo utawakutanisha viongozi mbalimbali ikijumuisha Mawaziri wa sekta mbalimbali, mabalozi kutoka nchi washirika wa maendeleo, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akisalimiana na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milisic, alipowasili kufungua mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa majadiliano ya kimkakakti kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutub, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa majadiliano ya kimkakakti kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban, akifuatilia majadiliano wakati wa mkutano wa majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini Bw. Zlatan Milisic, akizungumza wakati wa mkutano wa majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam, ambapo aliahidi kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
Mkutano ukiendelea wa majadiliano ya kimkakakti kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam, ambao umewakutanisha wataalamu kutoka Serikalini na Washirika wa Maendeleo kutoka ofisi za balozi mbalimbali nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Washirika wa Maendeleo wakati wa mkutano wa majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.
Kamishina wa Fedha za Nje Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Sauda Msemo akifuatilia mawasilisho wakati wa mkutano wa majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es salaam.(Picha na Wizara ya Fedha na Mipango Dar es Salaam).
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment