SHEIKH KABEKE AWATAKA VIONGOZI KUWA NA HOFU YA MUNGU | Tarimo Blog

 NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza


SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke, amewataka viongozi wa serikali waliopewa dhamana ya kuwatumikia Watanzania, wawe na hofu ya Mungu,wajiepushe na vitendo vya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na rushwa.

Alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa baada ya sala ya Idd iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana,jijini Mwanza.

Alisema wapo watu ambao ni viongozi serikalini wameaminiwa na kupewa dhamana ya kuwahudumia Watanzania lkini kwa kukosa hofu ya Mungu wanatenda kinyume badala ya kutenda ama kufanya mambo kwa maslahi ya umma.

“Nitumie fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, ameanza vizuri katika kuhakikisha anaipeleka Tanzania na wananchi kwenye maendeleo,lakini wapo watu wameaminiwa na kupewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, wanafanya kinyume,”alisema Sheikh Kabeke na kuongeza;

“Hawa hawana hofu ya Mungu, mtu aliyelelewa kwenye maadili ya dini na kumcha Mungu hawezi kula rushwa wal kutoa rushwa, mtoa rushwa na mpokeaji wote wataingia motoni,kwa vile wameaminiwa kwa niaba ya umma watende kwa uadilifu na haki.”

Alieleza kuwa Hayati Rais John Magufuli alimtumaini Mungu katika utendaji na maisha yake,alijipambanua kwa ucha Mungu na alionyesha bayana kuchukizwa na vitendo vya ufisadi,rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Hivyo ili taifa lisonge mbele watu waliopewa dhamana ya uongozi serikali ili kutumikia umma, wawe na hofu ya Mungu, watende kwa unyenyekevu na uadilifu pamoja na kujiepusha vitendo viovu vinavyoinyong’onyeza jamii hasa wananchi masikini. 

Aidha aliwaonya waislamu kujiepusha na mtego wa wanaobeza kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi na kuwataka wakasome hadithi za Mtume na kuzingatia mambo manne yaani Quran,Hadithi za Mtume, Ijimaa na Kiasi.

“Tusikubali kuingia kwenye mtego ambao hatumo, nani kawaambia mwanamke hawezi kuwa rais? Tuache propaganda za kupotosha,tumuunge Mkoa Rais Samia Suluhu Hassan na kumwombea na kumsaidia kwa anayoyafanya maana mtu yeyote anayemtukuza mwanamke ataitwa mheshimiwa na atakaye mdhalilisha mwanamke atadhalilika (atadhalilishwa),”alisema Sheikh Kabeke.

Alikumbusha Mke wa Mtume alikuwa mwalimu wa masahaba na Bi.Hajira alikuwa mwanamke aliyeasisi ibada.

Katika hatua nyingine,Mkurgenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alisema nidhamu miongoni mwa waislamu imepungua jambo linalosababisha wasifanikiwe.

“Kukosa nidhamu na kutowaheshimu viongozi dini ni udhaifu mkubwa, Sheikh wa Mkoa (Kabeke) amebeba dhamana ya waislamu ahera na duniani,ataulizwa/wataulizwa walitusimamiaje na sisi tutaulizwa tuliwatii na kuwaheshimu?” alihoji Kibamba na kueleza kuwa nidhamu ni mwanzo wa mafanikio na kwamba kila jambo linafanyika kwa mwongozo (kanuni) wa Mwenyezi Mungu.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, alisema waislamu wamekuwa msaada kwa jeshi hilo katika kutimiza majukumu yao kisheria katika misingi ya utu ili kudumisha amani na utulivu na kuwatakia waislamu waliojaliwa kufunga Mwezi wa Ramadhani kheri, moja ya nguzo ya dini hiyo na kuwataka waendelee kushikamana huku wakiepuka kufanya vitendo viovu na vya uvunjifu wa sheria ili kuepuka kusuguana na sheria


Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke, akitoa hutubabaada ya sala ya Idd iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Nyamagana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (ACP) Jumanne Muliro, akitoa salamu kwa waumini wa Dni ya Kiislamu jana baada ya sala ya Idd iliyofayika katika Uwanja wa Nyamagana.Picha zote na Baltazar Mashaka 
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza,Kiomoni Kibamba akitoa salamu za Idd kwa Waumini wa Kiislamu baada ya sala ya Idd jana kwenye Uwanja wa Nyamagana.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2