Shirika la WaterAid Tanzania lakabidhi miradi miwili ukiwemo wa uboreshaji miundombinu ya maji safi wa mazingira | Tarimo Blog

SHIRIKA  la Kimataifa la WaterAid Tanzania,limekabidhi miradi miwili ukiwemo wa  uboreshaji miundombinu  ya maji safi wa mazingira (Back to School Wash) na mradi wa kubadili tabia kwenye masuala ya mazingira na usafi binafsi (HBCC) iliyogharimu Sh Milioni 280.

Mbali na miradi hiyo,pia wamekabidhi jengo litakalotumiwa na  wanafunzi wa kike kwa ajili ya kujisitiri wakiwa katika hedhi,lililopo Shule ya Msingi Mringa wilayani Arumeru,Arusha.

Miradi hiyo ni ya  uboreshaji miundombinu  ya maji safi wa mazingira (Back to School Wash) na mradi wa kubadili tabia kwenye masuala ya mazingira na usafi binafsi (HBCC).

Miradi hiyo inatekelezwa na Shirika hilo katika wilaya za Arusha na Arumeru,inafadhiliwa na FDCO na Unilever.

Akizungumza leo wakati wa kukabidhi miradi hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Mt.Meru na Shule ya Msingi Mringa,Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WaterAid Tanzania,Anna Mzinga,amesema bado elimu inahitajika juu ya umuhimu wa unawaji wa mikono ili kuweza kujikinga na magonjwa ya milipuko.

Amesema kupitia mradi wa kampeni ya usafi HBCC uliotekelezwa jiji la Arusha wameweza kusanifu na kuweka miundombinu ya kunawia mikono katika maeneo sita  ya wazi ya mikusanyiko ikiwemo Hospitali ya Mt.Meru,masoko na taasisi za afya yaliyomo katika kata mbili.

Kuhusu mradi wa usalama wa afya wa mtoto wamejenga sehemu 11 za kuwania mikono katika shule nane za msingi ambazo ni Oldonyosambu,Leminyor,Lemanyata,Selian,Lemanyata,Olosiva,Enaboishu na Mringa zilizopo katika Kata tano zilizopo wilayani Arumeru.

“Chimbuko la miradi hii miwili ni kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19,ambapo katika jitihada za kupambana na athari zake kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo tumefanikiwa kutekeleza miradi hii miwili Arusha iliyogharimu Sh Milioni 280,”amesema

Mkurugenzi huyo amesema katika mradi wa “Back to school”,umeweza kunuaisha wanafunzi zaidi ya 5,800 waliowezeshwa  miundombinu ya kunawa mikono katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya milipuko huku katika mradi wa HBCC ukiwafikia wananchi zaidi ya 21,000.

Amefafanua kuwa kati ya hizo Shule nane za msingi,katika shule hiyo ya Mringa ni tofauti  kwani wamechangia nguvu katika  jitihada za mpango wa uboreshaji wa huduma ya afya ya mtoto wa kike kwa kukamilisha jengo maalum la sitara kwa wasichana wakiwa katika hedhi,”

Mbali na mkoa wa Arusha maeneo mengine ambayo mradi wa ‘Back to School’,unatekelezwa ni pamoja na Zanzibar,Dar Es Salaam na Geita,ambapo wamelenga hasa maeneo yenye miji mikubwa kwa kuangalia maeneo ambayo athari ya magonjwa ya milipuko ingeweza kuwa kubwa.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mt.Meru,Dk.Kipapi Mlambo,ameshukuru wadau hao kwa kuwezesha miradi hiyo na kuwa wagonjwa wanaoingia na kyoka hospitalini hapo wanatumia vifaa hivyo.

“Tunashukuru sana kwani hivi sasa watu wameelimika juu ya umuhimu wa kunawa mikono lengo likiwa ni kupunguza na kujilinda juu ya magonjwa ya milipuko,”

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha,Agnery Chitukulo,amesema bado kuna uhitaji wa vifaa hivyo vya kunawa mikono katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo shule,hospitali,zahanati,masoko na vituo vya afya.

"Tunashukuru ni vifaa vya kisasa na vyenye ubora wa hali ya juu,nitoe wito kwa wenzetu wa WaterAid,mkoa wetu wa Arusha bado una uhitaji mkubwa wa vifaa kama hivi tunavyo vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali,zahanati na vituo vya afya 393,Shule tunazo zaidi ya 800,masoko maeneo yote yanahitaji huduma kama hizi hasa kipindi hiki ambacho tuna changamoto ya Covid 19,"

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mt.Meru,Dk.Kipapi Mlambo,amesema wamepiga hatua katika hatua za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza tangu kuwekwa kwa vifaa hivyo.

"Tumepiga hatua katika kujikinga kwa ujumla na magonjwa ya kuambukizwa hasa yanayoanzia kwenye unawaji wa mikono,tutoe shukrani ya pekee kwa WaterAid kwa vifaa hivi na watu wanahamasika kila anayeingia na kutoka lazima anawe mikono,"







 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2