Charles James, Michuzi TV
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi yake ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania (TEWW) inatoa wito kwa watanzania wenye sifa za kujiunga na Vyuo vyao kufanya udahili mapema kabla ya muda wa dirisha la udahili uliopangwa kufungwa.
Kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na Taasisi hiyo kwa ngazi ya Stashahada dirisha lao la udahili limeshafunguliwa kuanzia Mei 15 huu na litafungwa Septemba 8, mwaka huu huku wale wa ngazi ya Shahada dirisha lao likifunguliwa Juni mwaka huu.
Akizungumza na Michuzi TV, Afisa Udahili wa TEWW, Justine Mbwambo amesema Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ni taasisi ambayo pamoja na mambo mengine inaandaa wataalamu wa elimu hiyo ya watu wazima nchini.
Amesema katika kutimiza jukumu hilo taasisi hiyo Ina programu ya elimu ya watu wazima na maendeleo ya jamii, elimu ya watu wazima na mafunzo endelezi katika ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada kwa njia ya ana kwa ana na njia ya mtandao.
Mbwambo amesema TEWW inaandaa wataalamu wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini ambao wana jukumu la kuanzisha, kusimamia na kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ya kielimu katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo Cha Umma na Maendeleo ya Wanawake kutoka taasisi hiyo, Leonia Kassamia amesema TEWW imekua ikianzisha na kusimamia mipango na miradi ya kielimu inayolenga makundi tofauti tofauti ya jamii ikiwemo vijana, watu wazima, wanawake na makundi mengine yenye mahitaji mbalimbali ya kielimu.
" Tuna miradi mingi ambayo tunaitekeleza na imekua msaada mkubwa kwa watanzania, tuna Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana (MECHAVI), Elimu Changamani Baada ya Msingi (MECHAM), Elimu ya Sekondari nje ya mfumo rasmi pamoja na kuwawezesha wasichana na wanawake walio nje ya Shule kupata elimu kulingana na mahitaji.
Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu maarufu kama IPOSA ni mradi unaolenga kutoa stadi za kisomo (kuandika, kusoma na kuhesabu),ujasiriamali, stadi za kazi na stadi za maisha," Amesema Kassamia.
Amesema kuwa mradi huo unatokana na kubainika kuwa kuna vijana wa umri wa miaka 14 hadi 17 wapatao Milioni 3.5 kwa sensa ya mwaka 2012 ambao hawako shuleni na hapakuepo programu thabiti ya kuwahudumia.
Kassamia amesema kuwa mpango wa IPOSA unawalenga vijana wa kike na kiume ambao hawajawahi kwenda Shule kabisa au wale walioacha kwa sababu mbalimbali za kimaisha.
" Mpango huu unatekelezwa kwa majaribio katika Mikoa Nane Nchini ambayo ni Kigoma, Dar es Salaam, Songwe, Tabora, Njombe, Iringa, Mbeya na Dodoma programu hiyo itaanza hivi karibuni," Amesema Kassamia.
Amesema miradi mingine inayotolewa na taasisi hiyo ni pamoja na kuwawezesha wasichana na wanawake walio nje ya shule kupata elimu kulingana na mahitaji yao ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuendeleza biashara ambapo mradi huo unatekelezwa katika Wilaya za Sengerema, Ngorongoro na Kasulu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment