Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Uchukuzi) Bw, Gabriel Migire amewataka wafanyakazi wa TAA kuhakikisha wanatumia rasilimali vizuri kulingana na sheria , miongozo na taratibu zilizopo ili kuondoa hoja za ukaguzi zinazoweza kutokea.
Bw, Migire alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dk. Leonard Chamuriho katika ukumbi uliopo katika jengo la PSSSF Jijini Dar Es- Salaam.
“Wafanyakazi wa umma wanapaswa kuhakikisha wanafanya matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo ili kuondoa hoja za ukaguzi , watumishi mnapaswa kufanya yale ya msingi yanayotarajiwa na wadau mbalimbali hata wa Kimataifa na pia mhakikishe Taasisi ina jina zuri kutokana na utendaji kazi wenu" amesema Bw, Migire.
Akizungumzia Mpango Mkakati wa mwaka 2021/2022 - 2025/2026 na bajeti ya mwaka 2021/2022 ya TAA iliyowasilishwa katika baraza hilo, Bw. Migire alisema, katika maandalizi ya bajeti na Mpango Mkakati ni vema kuweka misingi ambayo itawezesha mambo mengine yote ya kiutendaji yaende vizuri na baadae kufanyiwa tathmini ya namna ya utekelezaji wake.
Aidha alisisitiza kuwa mipango ya Taasisi si ya viongozi tu bali ni ya watumishi wote kwa pamoja na bila hivyo ni kupoteza muda na rasilimali fedha za umma.
Hata hivyo, Bw, Migire amesema ni imani yake kuwa maandalizi hayo ya bajeti yalienda kwa kufuata miongozo iliyowekwa na kuhakikisha agenda za Kitaifa zinatafsiriwa vema katika maeneo ya kazi huku akiwataka wajumbe waelewe vizuri bajeti hiyo na kwenda kuitekeleza na kutenda haki maana bajeti ni takwa la kisheri.
Awali akimkaribisha Bw. Migire Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Mhandisi Mshauri Julius Ndyamukama alisema, Ufanisi wa Mamlaka katika kipindi cha miaka ishirini na moja iliyopita umekuwa ni wa kuridhisha kutokana na maboresho ya miundombinu , ununuzi wa vifaa vya uendeshaji na ubora wa huduma huku mapato yakiwa yameongezeka kutoka bilioni 4.2 kwa mwaka 1999/2000 hadi kufikia shilingi bilioni 101.4 kwa mwaka 2019/2020.
Vilevile, TAA imefanikiwa kuthibitishwa katika ISO katika maeneo matatu ya ithibati, ambayo ni ISO 9001:2015; 14001:2015 na 45001:2018) ya Quality Management System: Environment Management System: Occupational Health and Safety System.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Ndyamukama alisema TAA inakabiliwa na baadhi ya Changamoto ikiwemo ya upungufu wa Wafanyakazi na gharama kubwa za utwaaji na umiliki wa maeneo ya Viwanja vya ndege huku akiiomba Wizara kuweza kusaidia katika changamoto hizo.
Mkutano huo wa 26 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi unafanyika kwa siku mbili kuanzia Tarehe 7- 8 Mei 2021 katika Ukumbi uliopo Jengo la PSSSF, Jijini Dar Es Salaam ukijumuisha Wajumbe Kutoka Kanda mbalimbali za TAA nchi nzima na unatarajiwa kufungwa tarehe 8 Mei, 2021.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment