Na John Nditi, Morogoro
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Shirika la Kusaidia Sekta Binafsi ya Kilimo ( Wakfu wa PASS) kimeanzisha Kituo Atamizi cha Vijana kinachoendesha mradi wa kulea na kufundisha vijana ujasiriamali kwenye sekta ya kilimo -biashara ili waweze kuongeza kipato chao na taifa kwa ujumla.
Kwa sasa kituo hicho kina vijana 92 ambao ni wahitimu wa Vyuo Vikuu , Vyuo vya Kati na Shule za Msingi waliojiunga tangu mwezi Oktoba na Novemba mwaka jana wakishiriki kufundishwa kwa kipindui cha mwaka mmoja.
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Profesa Raphael Chibunda alisema hayo mbele ya mkuu wa Chuo Kikuu hicho Jaji Mstaafu , Joseph Warioba pia ni Waziri mkuu Mstaafu wakati wa mahafali ya 37 ya kati kati ya mwaka (2021) ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine ( Kampasi kuu) mjini Morogoro.
Katika Mahafali hayo jumla ya wahitimu 149 kati yao wanaume 92 na wanawake 57 walifauli kutunukiwa vyeti vya kuhitimu masomo yao kwenye ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya kwanza , Shahada ya Umahiri, Shahada ya Uzamivu (PhD) ambao walikuwa 15 na kati yao wanawake ni watano.
Profesa Chibunda alisema , Miundombinu iliyojengwa kwenye Kituo Atamizi ni pamoja na vitalu nyumba 87 kati ya 100 na maeneo ya mashamba kwa ajili ya kilimo cha nje , miundombinu ya maji kwa ajili ya umwagiliaji.
“ Lengo la Kituo hiki kwa ajili ya kuzalisha mazao kibiashara chini ya uangalizi maalumu na kuwafundisha vijana wanaohitimu kutoka vyuo vya elimu ya juu , kati na shule za msingi nchini” alisema Profesa Chibunda.
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu hicho alisema ;Vijana hawa wanapohitimu kutoka kwenye Kituo hiki waweze kwenda kubadirisha sura ya kilimo cha nchi yetu ili kuwe na tija zaidi katika kuchochea ukuaji wa uchumi “ alisema Profesa Chibunda.
Katika hatua nyingine alisema, kwa kipindi cha mwezi Januari, 2021 hadi sasa, Chuo kimepata miradi mipya nane ya utafiti yenye thamani ya Sh bilioni 2.2 na imefadhiliwa na wadau mbalimbali kutoka ndani nan je ya nchi.
Hata hivyo alisema , Chuo kinaendelea kutekeleza mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo ya taaluma , utafiti , ugani na miradi ya maendeleo na Taasisi nyingine za ndani nan je ya nchi zaidi ya 90.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman alisema, katika kusimamia urekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chuo wa awamu ya nne 2016-2021 ulioanza kutekelezwa Julai 1, 2016 hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 74.45 na kutumika Sh milioni 39.95.
Pia alisema, kwa niaba ya Baraza la Chuo hicho anaishukuru Serikali kwa ruzuku na fedha za maendeleo inayotoa kwa Chuo, kwani ni dhahiri bila fedha hizo kisingeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuwaasa wahitimu wa Chuo hicho kuwa wakatumie elimu walioipata katika kujenga Taifa letu ,na wawe wenye nidhamu na uadilifu katika kazi zao za kila siku.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment