WAKAZI MBAGALA KONGOWE WAPATIWA ELIMU YA HUDUMA KWA WATEJA | Tarimo Blog



Afisa Huduma kwa Wateja Mkoa wa Kihuduma Mbagala Safina Muki akitoa elimu kwa wananchi na watumiaji wa maji baada ya kuwatembelea na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali.
Afisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) David Nkulila  akitoa elimu ya huduma kwa wateja kwa wananchi Mbagala Kongowe waliokuwa wanapata huduma kutoka Jumuiya za Maji Kongowe.
Baadhi ya wananchi wa Mbagala Kongowe wakiuliza maswali wakati wa Mkutano wa utoaji elimu ya huduma kwa wateja kutoka Dawasa.
 


Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

WAKAZI wa Mbagala Kongowe wamepatiwa  elimu ya huduma kwa wateja kutoka kwa maafisa wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Dawasa imetoa elimu hiyo kwa wakazi wa Kongowe waliokuwa wanahudumiwa na jumiiya za maji Kongowe na kwa sasa watakuwa wanahudumiwa na mamlaka hiyo kupitia Mkoa wa Kihuduma Mbagala.

Akizungumza na wananchi hao, Afisa huduma kwa wateja Mkoa wa Kihuduma Mbagala Safina Muki amesema Dawasa inaendelea kutoa huduma kwa wateja wote waliokuwa wanapata huduma ya maji kupitia Jumuiya za maji.

Muki amesema," leo tumekuja hapa kutoa elimu ya huduma kwa wateja na wananchi wanatakiwa kutambua wana haki ya kupata taarifa zote kutoka kwetu sisi Dawasa na tunapokea malalamiko yenu kupitia namba za huduma kwa wateja,"

Amesema, wanafahamu changamoto zilizopo kwa sasa maji hayatoshelezi ila kuna miradi mikubwa ya maji ipo katika ujenzi na itakapokamilika kero ya maji kwa wananchi wote wa Kongowe na Mbagala nzima itaondoka.

Aidha,  Muki amesema wanafahamu Kongowe kuna cchangamoto zilizokuwepo kabla ya Dawasa na bado zipo ila Ofisi ya Mkoa wa kihuduma inaendelea kushughulikia ikiwemo kurekebisha miundo mbinu iliyopo na kubadili mita za maji.

Hata hivyo, amesema kwa saaa mfumo wa kutumiwa ankara ya maji umebadilishwa na wateja wanaopata huduma kutoka Dawasa watakuwa wanatumiwa katika tarehe 20 hadi 30 ya mwezi na mteja atatakiwa kulipa kabla ya ankara ya mwezi unaofuata.

Kwa upande wa Afisa Mawasiliano Dawasa David Nkulila amewataka wananchi wa Kongowe kutoa taarifa zao kwa wahusika kupitia namba za huduma kwa wateja au Meneja wa Mkoa ili kusikilizwa kero zao.

Nkulila amesema, Dawasa ina muda mchache toka ikabidhiwe mradi huo ila inahakikisha malalamiko yote ya wateja yanafanyiwa kazi kwa wakati na kuwataka kupiga simu au kufika kwenye ofisi za Dawasa kwa maelezo zaidi.

Nao wananchi wa Kongowe wameiomba Dawasa kushughulikia changamoto zao kwa haraka na hata wakiwapigia simu wafike kwa wakati kwasababu maji yanavyomwagika yanatia hasara serikali.

Wameomba, kuongezewa kwa tanki la kuhifadhia maji kwani lililopo lina ujazo lita za ujazo 5000 halitoshelezi kwa wateja wote wanaopata huduma kutoka Dawasa kupitia mradi uliokuwa wa jumuiya za maji.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2