NAIBU Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekul amewataka wasanii nchini kuitangaza Makumbusho ya Taifa Tanzania ili watu wengi watembelee na kujifunza kuhusu urithi adhimu wa kitamaduni na Asilia
Wito huo ameutoa alipokuwa akifungua onesho la Museum Art Explosion "HOODI GEREZANI Kazi Kitamaduni" la mwezi Mei mwaka huu katika Ukumbi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar Es Salaam.
Mhe. Gekul licha ya kuushukuru uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa ubunifu wa program mbali mbali zinazo toa fursa ya uhifadhi wa mazao ya Utamaduni hususani Sanaa aliwasisitizia wasanii nchini kutumia fursa hiyo muhimu ili iwe chachu ya mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
"Makumbusho ya Taifa kuna vitu na taarifa nyingi muhimu zinazo husu Taifa letu, nimuhimu sana kwa wasanii tunapokuja hapa tuwe mabalozi wa kuitangaza Taasisi hii ili watu waje wajifunze Uzalendo, Umoja na Mshikamano na wapi tulipotoka na tulipo ili Tanzania iendelee kuwa na watu wenye uelewa mpana juu ya thamani ya Utanzania wetu". Aliongezea Mhe Gekul.
Mhe Gekul aliendelea kwa kusisitiza kuwa Wizara yake inatambua Mchango mkubwa wa Makumbusho ya Taifa katika uhifadhi wa urithi wa Utamaduni hivyo wataendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha Taasisi hiyo inatangazwa zaidi na mchango wako unafikia watanzania na wageni wengi zaidi.
Akimshukuru Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam Bw Achilesi Bufure, alisema Program ya MAE mwezi huu imelenga kuelimisha jamii juu ya mchango mkubwa unaotolewa na Jeshi la Magereza katika kuwapatia ujuzi Wafungwa ili wanapo rudi uraiani waweze kuutumia kama njia ya kujipatia kipato pia kuondoa hisia mbaya miongoni mwa watu kuhusu Jeshi la Magereza nchini.
Naye Raisi wa Shirikisho la Wasanii wa Sanaa za Ufundi nchini Bwana Adrian Nyangale aliushukuru uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuendelea kushirikiana na wasanii nchini katika kuhakikisha wanapata nafasi ya kuonesha mazao ya Utamaduni Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kupitia MAE na Kijiji cha Makumbusho kupitia program ya Kijiji Soko.
"Kwa kweli Makumbusho ya Taifa inafanya kazi nzuri sana, tunaahidi tutaendela kushirikiana nayo bega kwa bega ili jamii iwe na uwelewa mpana juu ya Makumbusho yetu na kuendelea kuthamini kazi za wasanii na wasanii nchini." Alisema Bw Adrian.
Makumbusho ya Taifa imeanzisha program mbali mbali za Sanaa na Utamaduni ili kutoa fursa ya wasanii kuonesha kazi zao kwenye kumbi na viwanja vya Makumbusho ya Taifa lakini pia kuhakikisha maonesho hayo yanakuwaj chachu ya Ujenzi wa Misingi imara ya Tunu muhimu za Taifa letu kama vile Amani, Umoja wa Kitaifa, Upendo, Mshikamano na Muungano wetu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment