Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amejitosa kuzungumzia mjadala unaondelea nchini baada ya kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga uliopangwa kufanyika Mei 8 mwaka huu katika Uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.
Majaliwa ameamua kuzungumzia mjadala huo ikiwa imepita siku mbili tu tangu kuahirishwa kwa mchezo huo na kuibua majadiliano kila kona ya nchi ya Tanzania na nje ya mipaka kutokana a ukubwa wa timu hizo ambazo zimebeba taaswira ya soka nchini.
Akizungumza leo Mei 10,2021 Bungeni Mjini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hivi;"Nimesimama kufuatia kero iliyojitokeza siku ya tarehe 8 mwezi huu kwa wanamichezo hasa wapenda mpira wa miguu baada ya kuahirishwa kwa mchezo wa jadi Simba na Yanga uliotakiwa kuchezwa siku hiyo.
"Na kusababisha manung'uniko , mijadala kwenye mitandao ya kijamii lakini pia kutojua hatma ya waliolipa viingilio kwa ajili ya mchezo huo.Jambo hili limevuta hisia za watanzania hata nje ya nchi kwasababu timu hizi ndizo zimebeba taaswira ya michezo nchini Tanzania."
Majaliwa amesema kutokana na kero hiyo tayari wametoa maagizo kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha wanatoa taarifa haraka kwa Watanzania, mchezo wenyewe unachezwa lini."Lakini pia vile viingilio hatma yake nini, naomba nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania na hasa wapenzi wa michezo kwenye eneo la mpira wa miguu ambao walijiandaa kuona, kusikia lakini kutoa viingilio kwamba tuipe muda Wizara ije kutoa ufafanuzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazosimamia michezo."
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment