Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema, Afisa Malalamiko yeyote katika Taasisi ya Umma ambaye anashindwa kutunza siri za malalamiko yanayowasiliswa kwenye dawati lake anapoteza sifa ya kuwa Mtumishi wa Umma muadilifu.
Dkt. Michael amezungumza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka zake za Serikali za Mitaa ambao wamepewa dhamana ya kushughulikia malalamiko ya wananchi katika taasisi zao.
Dkt. Michael amesema Maafisa Malalamiko katika Taasisi za Umma wanapaswa kujenga imani kwa watumishi na wananchi wanaowasilisha malalamiko kwenye ofisi zao kwa kutunza siri zinazohusu malalamiko yanayowasilishwa.
Amefafanua kuwa, uvujishaji wa siri zinazohusu malalamiko yaliyowasilishwa ni ukiukwaji wa Kanuni Na. 8 ya Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005 ambayo inawataka Watumishi wa Umma kutunza siri zinazohusu utekelezaji wa majukumu yao.
Dkt. Francis ameongeza kuwa, Afisa Malalamiko hapaswi kuwa na upendeleo wakati wa kushughulikia malalamiko, na badala yake anapaswa kuwa mshauri kwa watumishi na wananchi wanaowasilisha malalamiko katika ofisi yake.
Sanjari na hayo, Dkt. Michael ametoa wito kwa Maafisa Malalamiko kutoa namba za simu za kiganjani ili kutoa fursa kwa watumishi na wananchi wenye malalamiko kuyawasilisha na kufanyiwa kazi.
Aidha, ametoa maelekezo kwa waajiri wote nchini kusimamia Utekelezaji wa Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Malalamiko ya Wananchi katika Utumishi wa Umma wa Mwaka 2012 ili kuhakikisha ofisi au dawati la ushughulikiaji wa malalamiko linakuwepo kwenye taasisi zao, ikiwa ni pamoja na kuwateua watumishi wenye sifa stahiki kushughulikia malalamiko ya wananchi.
Awali akimkaribisha Dkt. Francis kufungua mafunzo hayo kwa Maafisa Malalamiko, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika alisema, mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji maafisa wanaoratibu ushughulikiaji wa malalamiko ili wafahamu namna wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao.
Bi. Leila ameongeza kuwa, maafisa hao watapata mafunzo kuhusu utekelezaji wa Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Malalamiko,uandaaji wa taarifa za malalamiko na watapewa elimu kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, haki na wajibu, dhana ya Utawala Bora, namna ya kuwahudumia na kuwadhibiti walalamikaji wa aina mbalimbali.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Idara ya Ukuzaji Maadili inatoa mafunzo ya siku tatu ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi yanayohudhuriwa na Maafisa Malalamiko kutoka Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa na Mamlaka zake za Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kwa maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi na CBE.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu na Maboresho, Ofisi ya Rais-Ikulu Bw. Apolinary Tamayamali akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael mara baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo kufungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika akieleza lengo la mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya Wananchi katika Utumishi wa Umma yanayotolewa kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa.
Baadhi ya Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko kwa maafisa hao yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment