KAMATI MAALUM INAYOSIMAMIA UCHAGUZI MKUU NaCoNGO YAHAMASISHA MAKUNDI YA WANAWAKE,VIJANA ,WATU WENYE ULEMAVU KUSHIRIKI | Tarimo Blog


Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa viongozi (NaCoNGO) Wakili Flaviana Charles ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea Haki za Binadamu na Biashara, (wa pili kulia) akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wao na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam. (kulia kwake) ni Katibu wa Kamati hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga, (wa kwanza kushoto) ni mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la (WISE) Dkt. Astronaut Bagile, na (wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi Shirika la (WiLDAF) Wakili Anna Kulaya.
Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa viongozi (NaCoNGO) Wakili Flaviana Charles (kulia) akijadiliana jambo na Katibu wake Francis Kiwanga (kushoto) wakati wa mkutano wao na waandishi wa Habari uliofanyika Juni 16, 2021.

Katibu wa Kamati hiyo Francis Kiwanga (aliyesimama) akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari kwenye Mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

KATIKA kuelekea kufanyika uchaguzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), unaotarajiwa kufanyika Julai 8 mwaka huu, Kamati maalum ya kitaifa inayoratibu na kusimamia uchaguzi huo imetoa mwito kwa makundi mbalimbali hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza kushiriki uchaguzi huo.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Uchaguzi huo Wakili Msomi Flaviana Charles, amesema kuwa uchaguzi huo umeitishwa mara baada ya kuundwa kwa kamati hiyo yenye watu 10 kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), ya kitaifa na kimataifa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ili kusimamia mchakato huo.

Ameongeza fomu za kuomba kugombea katika nafasi mbalimbali  zitaanza kuchukuliwa rasmi  Juni 21 katika Ofisi zote za Afisa Maendeleo ya Jamii  wa wilaya zote 139 nchini na mwisho wa kurudisha fomu hizo ni Juni 24 mwaka huu.

Aidha ameongeza kuwa ifikapo Juni 25,mwaka huukutafanyika mchakato wa kuchakata fomu zote za wagombea katika Ofisi hizo na kazi hiyo itafanywa na  kamati hiyo.

"Ifikapo Juni 26,2021 uchaguzi katika ngazi za wilaya utaanza huku Juni 28 uchaguzi wa wajumbe wa Baraza katika ngazi ya mkoa ambapo Julai 5 hadi 8,2021 utakuwa ni uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa baraza, kamati ndogo na wajumbe wa bodi ya uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali,"amesema  

Amesema Julai 9 hadi 10 mwaka huu kutakuwa na uapisho na makabidhiano ya nyaraka na Ofisi na kuanza kazi kwa watumishi hao. Wakili Flaviana amewalihimiza watu wote wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo kujitokeza kugombea nafasi hizo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na makundi maalum yakiwemo ya watu wenye ulemavu. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Foundation for Civil Society, (FCS) Francis Kiwanga  amesema kuwa  Baraza hilo ni muhimu katika Taasisi hususani katika kazi zote hizo za kusimamia masuala ya uchaguzi.

"Rai yetu sisi kwa Asasi zote za Kiraia kila mtu aweze kushiriki na watu wachukue fomu na kugombea nafasi hizi zilizotangazwa ,"amesema na kuongeza. "Ushiriki wa wanawake katika uchaguzi huu ni muhimu sana hivyo tunatoa Rai yetu watu wajitokeze ili baraza liwe shirikishi zaidi na wadau wenye upana,"amesema  Kiwanga.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2