Makinda amrithi Salim Ahmed Salim HKMU | Tarimo Blog

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki (HKMU), John Ulanga akimvalisha kofia Mkuu mpya wa  Chuo hicho, Anne Makinda kama ishara ya kumsimika rasmi kwenye nafasi hiyo. Makinda anachukua nafasi ya Salim Ahmed Salim. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi  wa Shirika la Afya na Elimu la Kairuki, Kokushubila Kairuki.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), wakiongoza maandamano ya kwenda kumsimika rasmi mkuu mpya wa chuo hicho, Anne Makinda kwenye hafla iliyofanyika  jana chuoni hapo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Spika mstaafu Anne Makinda akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa HKMU mara baada ya kusimikwa rasmi kuwa mkuu wa chuo hicho kwenye hafla iliyofanyika jana Mikocheni jijini Dar es Salaam..
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Spika mstaafu Anne Makinda akiongoza kwenda kwenye hafla ya kumsimika rasmi kuwa mkuu wa chuo hicho jana jijini Dar es Salaam Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, John Ulanga na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi  wa Shirika la Afya na Elimu

Na Mwandishi Wetu
SPIKA mstaafu, Anne Makinda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) akichukua nafasi ya Salim Ahmed Salim.

Hafla ya kumsimika rasmi kwenye nafasi hiyo imefanyika leo Juni 18,2021 chuoni hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo hicho kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salam.

Akizungumza mara baada ya kusimikwa nafasi hiyo, Makinda amesistiza maadili na nidhamu kwenye vyuo vikuu hususani vinavyotoa elimu ya tiba na uuguzi, kwa kuwa itasaidia wahitimu wa kada ya afya kutoa huduma zilizo bora na haki.

Pia amesema vyuo hivyo hususani vya binafsi, vibadili changamoto za kiuchumi walizonazo na kuwa fursa, ili kuongeza ufanisi na ushindani uliopo kwenye soko.

Amesema mafunzo pamoja na vyeti pekee haitoshi kumtambulisha mhitimu wa chuo kikuu kuwa bora, bila ya kufuatwa kwa kanuni za maadili katika utendaji wao wa kazi za kuhudumia jamii.

“Nidhamu pekee inaweza kukifanya chuo kuwa chenye ubora, mafanikio pia yanatokana na nidhamu, huwezi kuwatendea visivyo wenzio ukiwa kwenye majukumu yako ukiwa na nidhamu. Nidhamu inaogopa.” Amesema Makinda.

“Nilikutana na baadhi ya wanafunzi wa chuo hiki, nikaona kabisa kuna nidhamu, hiyo ni muhimu sana, nidhamu na maadili kwa wanafunzi ni kitu cha kwanza. Nilipokuwa India siku za nyuma, baadhi ya wadau waliniambia watafungua chuo cha wauguzi, kwa sababu wanasikia baadhi yao hawana nidhamu.”

“Pamoja na wahitimu wa sekta ya afya baadhi yao kutokuwa na ajira, bado watoa huduma hawa wanahitajika kwenye jamii na taifa kwa ujumla.”

Kadhalika, Makinda ametoa wito kwa chuo hicho kubuni vyanzo vya mapato, badala ya kutegemea chanzo pekee cha ada kutoka kwa wanafunzi, huku akishukuru chuo hicho kwa kumchagua kuwa mkuu wa chuo, akichukua nafasi ya Balozi Salim Ahmed Salim.

“Ni Mungu amenichagua kuwa katika nafasi hii, ingawa ukistaafu unahitaji kutulia na majukumu, nikakubali sababu najua Mungu kupitia chuo hiki ndio amenichagua. Lakini mimi nakawambia nawaangalia ninyi sababu historia ya hospitali hii naijua, mna ushirikiano, upendo na nia, licha ya kuondoka mwanzilishi, marehemu Kairuki.

“Mfumo aliouacha umefanya chuo hiki kiendelee kuwepo. Nidhamu na maadili naiona kwa wanafunzi wenu mnaowafundisha, hata ukiwa nje huko, kwa sababu masomo ni yale yale katika vyuo vingine ila ninyi mnanidhamu.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa chuo hicho, Kokushubila Kairuki, alisema kuwa anaiomba serikali iangalie namna ya kuvisaidia vyuo binafsi kwa kuwapatia fedha ili kuinua ufanisi wa vyuo nchini.

“Nina imani wahitimu wa vyuo binafsi, ikiwamo Kairuki wakitoka hapa wanakwnda kuhudumia jamii hivyo tunaiomba serikali isaidie kutoa fedha kwa vyuo binafsi. Pendekezo hili linaanzia kwa mkuu wetu mpya, Makinda, tunafahamu uzoefu ulionao katika uongozi na una ushawishi,” amesema.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2