RAIS WANGU MAMA SAMIA SULUHU HASSAN NIKWAMBIE TUNAKUELEWA, WATAKAOZINGUA KAMA KAWA WAZINGUE TU...KAZI IENDELELEE | Tarimo Blog



 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Pansiasi Jijini Mwanza wakati akielekea kuzindua Jengo la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza leo tarehe 13 Juni, 2021.

 

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

NIKIRI mapema huko nyuma sijawahi kuzungumza au kuelezea chochote kinachomuhusu mama yetu Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa sasa ndio Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hongera mama yetu, hongera Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera Mwanamke Jasiri, Mwanamke wa nguvu, Malkia wa nguvu ,tangu uwe Rais wetu hakika unaiongoza nchi yetu vizuri, umeishika imeshikika.Hongera Rais.

Kama nilivyotangulia kueleza hapo kwenye utangulizi, sikuwahi kumuelezea Mama Samia, ndio kwanini niseme uongo? Kinachonifurahisha na kunipa ujasiri leo hii ni kwamba nimekuwa nikimfutilia kwa muda mrefu hasa tangu alipoanza kuongoza nafasi  mbalimbali za uongozi.

Ni mama kiongozi,  najua ana historia ndefu kwenye siasa baada ya kuamua kuingia huko akitokea kwenye mashirika binafsi ambako nako alifanya kazi nzuri.

Nimemsikia huko nyuma mara kadhaa wakati akielezea safari yake ya maisha hadi kuja kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015 baada ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM Hayati Dk. John Magufuli kupendekeza jina lake na chama kulipitisha.

Hata hivyo mimi nilianza kumfuatilia Mama Samia baada ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, hapo ndipo nilipoanza kumfutilia, alionesha umakini wa hali ya juu  kusimamia kikao cha Bunge la Katiba, Bunge ambalo lilikuwa na kila aina ya hoja na vihoja lakini bado Mama Samia hakuyumbishwa na wajumbe wa Bunge hilo.

Baadhi yao walikuwa wakijenga hoja za ovyo aliwasikiliza kwa makini na kisha kutoa maelekezo kwa hekima na busara. Nyota yake ilianza kung'aa hapo.Watanzania wa Bara na Pwani tukamjua, hata wale wasiomjua kuanzia hapo jina la Samia likawa vichwani mwao.

Alisimama imara kwenye nafasi hiyo, Bunge likaisha ,Mama akabaki na heshima ambayo haitafutika kwenye historia ya Taifa la letu, ni wazi mjadala wa Bunge la Katiba ulikuwa moto, hoja ya Serikali Moja, Serikali Mbili na hata Serikali Tatu hazikumtoa Mama Samia kwenye reli, alijua msimamo wa Chama chake cha CCM, alijua msimamo wa Serikali inayotokana na CCM.

Pia mama Samia alijua msimamo wa viongozi wa vyama vya siasa nchini na kubwa zaidi alijua mahitaji ya Watanzania kwa kada tofauti.Ndio kila mmoja alikuwa na lake.Hata hivyo uzuri Bunge hilo lilijaaa wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii yetu.

Nazungumzia Bunge la Katiba kwa sababu Mama Samia hapo ndipo alipothibitisha ana uwezo, anajua maana ya uongozi. Ndio wakati kijana mdogo kwa wakati huo Paul Makonda ambaye alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba aliposimama mbele ya wajumbe wengine na kueleza kwamba kwa jinsi Mama Samia alivyoonesha umahiri wake na ubora wake kwenye Bunge hilo,basi CCM ikiwapendeza huko mbele ya safari apendekezwe na kuwa Makamu wa Rais.Ni muda umepita sasa lakini utabiri ule wa Makonda ,ukatimia mwaka 2015.Bunge la Katiba lilikuwa katika utawala wa Awamu ya Nne ya Dk.Jakaya Kikwete.

Tangu wakati huo Mama Samia nyota yake ilizidi kung'aa machoni mwa Watanzania kutokana na haiba na kariba yake kwenye uongozi uliogeuka tunu kwa Watanzania.
Kwa kukumbusha tu Mama Samia amekuwa kwenye Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Dk. Jakaya Kikwete 'mzee wa Msoga' mzee asiyekuwa na makuu.

Jakaya asante kwa wakati wako ulioona haja ya kumjenga kiongozi Mama Samia.Najua huko mbele ya safari atakapoamua kuandika kitabu chake atakuelezea vizuri.

Hata hivyo msemo wa Wahenga Kizuri Kinajiuza umethibitika kwa Mama Samia, Hayati Dk.John Magufuli wakati anagombea kwa mara ya kwanza Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema kama atakuwa Rais basi Makamu wake wa Rais atakuwa Mama Samia.

Dk. Magufuli alifanya hivyo kwa kutambua sifa za uongozi za Mama Samia. Akiwa hai, ambapo  Rais Magufuli alimuelezea vizuri Mama Samia, alijivunia kuwa na Makamu wa Rais Mama Samia.Hivyo binafsi sina shaka na Mama Samia nchi yetu iko katika mikono salama.Sina shaka kabisa na Mama Samia.

Kuhusu Mama Samia na nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano aliipata baada ya Taifa letu kuondokewa aliyekuwa Rais wetu Dk.John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu wa 2021, kwa maradhi ya moyo, ambayo tulielezwa yalimsumbua kwa muda.

Kifo cha Dk. Magufuli kimetutikisa kama nchi, tumeumizwa, tumelia vya kutosha na sasa tunabakia tukimuombea Mungu ampe pumziko la milele.Lala Dk. Magufuli Watanzania tunakukumbuka.
 
Hata hivyo tunatabasamu maana umetuachia Mama Samia, mama uliyemuamini na kumpa nafasi kubwa katika nchi yetu.Mama Samia ameingia kwenye rekodi itakayoandikwa kwa kalamu ya wino wa dhahabu, ni Rais wa kwanza Mwanamke katika nchi yetu, pia ndio mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais nchini Tanzania,hongera mama.

Hakika mama ni baraka, mama ni mlezi, mama ndio mama. Nikuahidi Mama Samia tutashirikiana nawe kwa kila jambo.Hatutarudi nyuma, hatuna shaka na uwezo wako,ndio.Kweli tena. Wanaovimba wapasuke, potelea mbali.

Tangu amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea kuiongoza nchi yetu vizuri.Hotuba zake zimeendelea kutuaminisha kwa kauli na vitendo ulivyo kiongozi shupavu.

Hongera sana mama kwa kutuongoza vizuri. Nafahamu unaendelea kupanga safu zako za uongozi. Endelea mama, kikubwa nchi yetu isonge mbele. Mungu yu pamoja nawe, Mungu yuko pamoja nasi Watanzania.

Nafahamu kwenye wengi kuna mengi, wapo wanaokuchukulia poa kisa tu wewe ni mwanamke, hawajui ni wewe ni mwanamke wa shoka.Huna masihara , nakushukuru ulishaeleza wazi na waliosikia wamesikia. Umesema wewe ni Rais mwanammke lakini ndio Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania.Tumekusikia tena kwa sauti yako ya upole lakini yenye kishindo kikukuu.

Narudia tena ahsante mama ulisema na tumekusikia. Hata ile kauli yako ya "Ukinizingua tunazinguana" naiona kwenye utendaji wako. Usirudi nyuma, nenda mbele na Watanzania zaidi ya milioni 60 tuko nyuma yako. Nafahamu msemo wako ukizingua tunazinguana tayari umewakuta baadhi ya watumishi wakiwemo wwteule wako.Wamezingua,nawe umewazingua.

Wakati naendelea kuandika nimekumbuka na ile kauli yako kwamba  ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako. Ukweli hauko peke yako, upo pamoja na Watanzania.Na Watanzania tuko pamoja nawe,tutafika mbali.Bajeti yako ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sits,imenipa matumaini makubwa.Tutakwenda mbali,tuko wote.

Hata hivyo naomba niseme kidogo, binafsi nakerwa na taabia ya baadhi ya watu ambao kazi yao ni kutengeneza ajenda chafu,ajenda za hovyo.Ndio watu hao wamekuwa wakipotosha ukweli, kila kinachofanywa na Rais Samia utawasikia wakisema sio mawazo yake,katumwa . Wamekuwa wakimhusisha Rais Mstaafu Jakaya Kikwete .

Wanajitahidi kueneza propaganda hiyo kama sehemu ya kurudisha nyuma jitihadaza za Rais.Nachofurahi mama hana muda wa kuhangaika na watu hao.Tuache kuwa na dhana ya hovyo, Rais Samia yuko imara, atabaki kuwa imara na ataendelea kuwa imara.Lakini najiuliza kuna ubaya gani Rais Samia akisiliza mawazo ya Watanzania wakiwemo viongozi wastaafu kuna dhambi gani? Acheni manano yenu.Kha!

Mtanzania mwenzangu najua na wewe unajua baada ya Mama Samia baada ya kuapishwa kuwa Rais wetu amepanga safu yake vizuri, anao washauri wenye weledi mkubwa.Anaye Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ambaye wote hatuna shaka na uwezo, elimu, maarifa, hekima na busara na anafanya kazi nzuri.

Tunafahamu Waziri Mkuu wetu, Kassim Majaliwa anafanya kazi kubwa na nzuri ya kumsaidia Rais Samia.Narudia tena ,hebu tuache kujenga hoja dhaifu , nani asiyejua kwamba tunalo Baraza la Mawaziri ambalo nalo linajukumu la kumshauri Rais Samia kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele.

Tuna Bunge imara chini ya Spika Job Ndugai nalo liko kwa ajili ya kushauri Serikali.Tumuache Rais Samia afanye kazi ya kutuongoza watanzania.Tumuache aendelee na jukumu la kutekeleza miradi ya maendeleo.

Ninajua yapo mengi ya kumueleza Rais Samia ambaye tu mara baada ya kushika madaraka ametuonesha muelekeo wa Serikali yake,kazi anayoifanya tunaiona.Wapo wanaobeza lakini ameendelea kuwajibu kwa vitendo.Watamuelewa muda sio mrefu.

Najua wapo baadhi ya watu ambao kwa namna moja au nyingine wanajifanya manunda,wanajifanya vichwa ngumu.Eti  hawakubaliani na unayoyafanya, hao wasikupe tabu,wapo ,walikuwepo na wataendelea kuwepo.Wanachoshindwa kuelewa Rais Samia amekuwa Rais akitokea kwenye nafasi ya Makamu wa Rais.

Hivyo alipata nafasi ya kujua mengi na kushauriana mengi na aliyekuwa Rais.Anaijua nchi na watu wake vizuri.Huko nyuma tumekuwa na marais ambao walikuwa marais wakitoa kwenye uwaziri, nazungumzia Awamu ya Tatu,Awamu ya Nne na Awamu ya Tano.

Mama Samia amekuwa Waziri,amekuwa Makamu wa Rais kwa miaka sita na sasa ndio Rais.Kuna tofauti kubwa kati yake na watangulizi wake.Weka akilini.Hata hivyo nihitimishe kwa kukusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania....tuitikie wote Kazi iendeleeeee....

SIMU 0713 833822


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2