SEKRETARIETI YA MAADILI YATEMBELEA KIJIJI CHA MATUMAINI NA KUKABIDHI MISAADA | Tarimo Blog

Charles James, Michuzi TV

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma wametembelea kituo cha kulea watoto cha Kijiji cha Matumaini ambapo wamekabidhi mahitaji mbalimbali ikiwemo vifaa vya usafi, pampers kwa ajili ya watoto wadogo.

Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi hizo kwa watoto wanaolelewa kwenye kijiji cha Matumaini, Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, John Kaole amesema wametembelea kituo hiki kwa lengo la kuwapa faraja watoto hao lakini pia kuwakabidhi zawadi hizo.

Kaole ametoa pia rai kwa watanzania wa kada mbalimbali kutenga muda wao kwa ajili ya kuvitembelea vituo vinavyolea watoto wenye mahitaji kwa lengo la kuwafariji.

Amesema katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma wameamua kuungana na jamii kusherehekea maadhimisho hayo ambapo awali walifanya usafi na kutoa vifaa vya usafi katika soko la Majengo lililopo jijini Dodoma.

" Tunawapongeza watawa ambao ndio mnasimamia kituo hiki cha Kijiji Cha Matumaini, mnalea watoto hawa kwa upendo, zaidi ya yote mnawasaidia watoto hawa kupata elimu ambayo ni msingi mkubwa wa mafanikio kwenye maisha yao.

Nitoe rai kwa watanzania tuwe na utaratibu wa kutembelea vituo kama hivi, tuwatie moyo wanaowalea na watoto wenyewe, sisi kama Sekretarieti ya maadili tunaamini maadili ya viongozi yanaanzia tokea wakiwa wadogo, tuwapongeze uongozi kwa kusimamia pia maadili ya watoto wetu hawa," Amesema Kaole.

Kwa upande wake mmoja wa watawa wa Kanisa Katoliki ambao ndio wasimamizi wa kituo hiko, Sister Suzana Maingu ameishukuru Sekretarieti ya Maadili kwa kutenga muda wao na kuwatembelea sambamba na kukabidhi zawadi hizo.

Amesema mpaka sasa kituo hiko kimeshasaidia zaidi ya watoto 300 toka kilipoanzishwa mwaka 2002 ambapo wapo watoto ambao tayari wameshamaliza elimu na wengine wapo kwenye ajira mbalimbali wakiwemo Madaktari, Walimu na Wahandisi.

" Tunashukuru sana kwa ujio wenu, umekua faraja kwetu na kwa watoto, tunaamini ujio wenu pia utakua chachu kwa Idara zingine za serikalini, watu binafsi nao kwa wakati wao kutenga muda wa kutembelea pia," Amesema Sister Suzana.

Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, John Kaole akizungumza kwa niaba ya Sekretarieti hiyo walipotembelea watoto wanaolelewa katika kituo cha Kijiji Cha Cha Matumaini jijini Dodoma leo.
Mmoja wa Watawa wanaosimamia kituo cha Kijiji Cha Matumaini, Sister Suzana Maingu akizungumza wakati walipotembelewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, John Kaole akikabidhi zawadi walizowapelekea watoto wanaolelewa katika Kijiji Cha Matumaini, Anayepokea ni mmoja wa Watawa wa Kanisa Katoliki, Sister Alfonsina Shirima.
 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2