TANI 3,900 ZA MBEGU BORA ZA ALIZETI KUSAMBAZWA KWA WAKULIMA – NAIBU WAZIRI BASHE | Tarimo Blog

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe  amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imepanga kununua jumla ya tani 3,900 za mbegu bora za alizeti kwa ajili ya kuzisambaza kwa Wakulima; Ambapo watapewa kwa njia ya ruzuku ya nusu bei kwa kila aina ya mbegu.

Naibu Waziri Bashe  amekutana na Wadau wa zao la alizeti wakiwemo wenye viwanda vya kati na vikubwa katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.
Waziri Bashe amesema licha ya Serikali kutoa kiasi cha tani 3,900 za mbegu bora za alizeti lakini Wakulima watanunua mbegu hizo kwa asilimia 50 tu.

“Asilimia 50 ya mbegu bora zitagharamiwa na Serikali lakini bado Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) itaendelea na mkakati wa kuzalisha mbegu bora ambapo  bajeti ya ASA imeongezeka kutoka bilioni 5 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 10 mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za alizeti.” Amekaririwa Naibu Waziri Bashe.

Naibu Waziri Bashe ameongeza kuwa sambamba na kuongeza bajeti ya uzalishaji wa mbegu Wizara ya kIlimo inataraji kutangaza zabuni ambapo Sekta Binafsi (Wafanyabiashara) watakaoshinda zabuni hiyo watahusika katika kuagiza mbegu bora kiasi cha tani 3,900 kutoka nje ya nchi na kisha zitasambazwa kwa Wakulima kupitia wenye viwanda vikubwa na vya kati kwa makubaliano ili baada ya kuzilima; Mazao yao watayauza kwa Wasindikaji (Wenye viwanda).

Naibu Waziri Bashe amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa alizeti kama njia mojawapo ya kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ambapo taifa hutumia zaidi ya shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2