Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna (wa pili kulia) akikabidhi Ripoti ya Mwaka 2020 kwa Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Edwin Mhede wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao siku ya Ijumaa. Wanaoshuhudia ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki hiyo, Juma Kimori (kulia) na Mkuu wa Idara ya Sheria na Katibu wa NMB, Bi. Lilian Komwihangiro.
……………………………………………………………………
- Ni sawa na ongezeko la 43% ikilinganishwa na gawio lililolipwa mwaka 2019
Katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 21 uliofanyika Juni 4, 2021, wanahisa wa benki ya NMB, waliidhinisha gawio la TZS 137 kwa kila hisa sawa na jumla ya shilingi bilioni 68.5 kwa ajili ya mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2020.
Kiasi hiki kilichotengwa mwaka 2020 ni sawa na ongezeko la 43% kutoka TZS 48 bilioni zilizolipwa mwaka 2019. Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa benki kuongeza gawio kwa wanahisa wake.
Gawio hilo litalipwa kuanzia Juni 16 2021. Ongezeko la gawio linalolipwa linadhihirisha ufanisi mzuri wa matekelezo ya mikakati ya Benki kwa mwaka 2020 pamoja na mtaji imara wa Benki ya NMB.
Benki ya NMB imeendeleza ufanisi wake kiutendaji katika mwaka 2020. Faida ya Benki baada ya kodi iliongezeka kwa 45% na kufika TZS 206 bilioni mwaka 2020 kutokea bilioni 142 mwaka 2019 hivyo kuweka historia ya faida kubwa zaidi kutokea kwenye sekta ya benki nchini. Benki pia ilimaliza mwaka na uwiano bora zaidi wa gharama za uendeshaji na mapato ambao ulikuwa 51% huku uwiano wa mikopo chechefu ukiwa 5% mwishoni mwa Desemba 2020, uwiano wote ukiwa ndani ya viwango vinavyokubalika na mdhibiti na msimamizi wa sekta, yaani Benki Kuu ya Tanzania.
Hii inathibitisha mwendelezo wa mkakati wa Benki kuimarisha uendeshaji wa shughuli za benki kwa kudhibiti gharama na kupunguza vihatarishi kwenye ukopeshaji. Vilevile, ongezeko la ufanisi wa Benki katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 unaonyesha nidhamu katika kusimamia mikakati ya Benki hivyo kusababisha faida baada ya kodi kuongezeka kwa 33% ikilinganishwa na iliyopatikana katika robo ya kwanza mwaka 2020 kufikia TZS 65 bilioni katika robo iliyoishia Machi 2021.
Benki ina mizania imara, mtaji na ukwasi wa kutosha juu ya viwango vilivyowekwa ambavyo vyote viko juu na mamlaka ya udhibiti wa taasisi za fedha nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede alisema, “napenda kuwashukuru wanahisa wote wa Benki ya NMB kwa ushirikiano wao waliouonyesha na imani yao kwa Bodi na menejimenti ya Benki. Gawio lililo idhinishwa linadhihirisha tu utendaji mzuri unaoongeza thamani kwa wadau wetu. Tunaahidi kuendeleza juhudi hizi kuongeza faida kwa wanahisa wetu na jamii tunayoihudumia. Tutaendelea kuhakikisha tunatimiza ndoto na malengo yetu na wanahisa.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema “mwaka 2020 tulipata matokeo mazuri sana licha ya changamoto za kimazingira zilizokuwepo. Mwenendo wetu mzuri kwa mwaka 2021 unaeleza jinsi tunavyoendelea vyema kutekeleza mpango mkakati na kudhihirisha kuwa tumechagua njia sahihi. Tuna mizania imara na mtaji wa kutosha unaotupa uwezo wa kukua zaidi sokoni.”
Bi Zaipuna aliongeza kwamba “tutaendelea kujiimarisha katika misingi imara ya Benki kukuza biashara yetu ili iwe endelevu. Tutaendelea kujikita kutoa huduma bora zaidi, za kibunifu na zinazokidhi matarajio ya wateja na wadau wetu ambao tunajisikia fahari kuwahudumia.”
“Kutokana na hazina kubwa ya vipaji tuliyonayo na nidhamu ya utekelezaji mipango yetu, tutaendelea kusaidia kufanikisha kuboresha maisha na uchumi wa Tanzania katika utekelezaji wa ajenda yake ya maendeleo kwa kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa na faida nono kwa wawekezaji wetu. Nafurahi na kushukuru ushirikiano tunaoendelea kuupata kutoka kwa wateja wetu, wadau, na wabia na tunatarajia kuendelea kutoa huduma za kipekee kwao,” aliongeza Bi Zaipuna.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment