ACP MASEJO ATOA TAARIFA YA KIFO CHA MTUHUMIWA WA MAUAJI | Tarimo Blog


Na Abel Paul, Jeshi la Polisi Arusha

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo ameeleza kuwa Ijumaa 23.07.2021 huko katika kijiji cha Makiba wilayani Arumeru, kulitokea tukio la mtu aitwaye Jacob S/O Kideko  maarufu kwa majina ya Wami au Ramadhan Kichwaa  (43) mkazi wa Makiba kumkata mapanga askari Polisi H.2307 Police constable Damas Magoti na kusababisha kifo chake.

Amesema kuwa baada ya tukio hilo kutokea siku hiyo Usiku, mtuhumiwa huyo alikimbia na kutokomea kusikojulikana na walianza kumtafuta ambapo tarehe 27.07.2021 askari wa Jeshi la Polisi mkoani hapo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa amejificha mkoani Morogoro.

Kamanda Masejo ameeleza kuwa taratibu za kumsafirisha kumleta mkoani Arusha ili aweze kukabiliana na kesi yake ya mauaji zilifanyika ambapo baada ya kuingia Arusha mjini eneo la Kisongo mtuhumiwa huyo akiwa amefungwa Pingu mikononi aliamua kujirusha toka ndani ya gari lililokuwa kwenye mwendokasi mpaka chini na kusababisha kupata majeraha kichwani na michubuko katika mwili wake.

ACP- Masejo amesema Kufutia tukio hilo mtuhumiwa alikimbizwa  hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu lakini alifariki dunia wakiwa njiani.

 Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi zaidi toka kwa Madaktari pamoja na utambuzi toka kwa ndugu.

Aidha amesema kuwa imebainika kwamba, kabla la tukio la kumuua askari Polisi, marehemu Jacob S/O Kideko alikuwa anatafutwa na Jeshi la Magereza na kwamba tarehe 10.09.2008 alifungwa miaka miaka 15 kwa kosa la Unyang'anyi wa kutumia nguvu na kosa la pili la Shambulio na kutoroka chini ya ulinzi ambapo hukumu yake ilikuwa Mwaka mmoja hivyo kuwa na jumla ya kifungo cha miaka 16
Aidha mtuhumiwa huyo akiwa anaendelea kutumikia kifungo chake kilichotarajiwa kumalizika mwaka 2026, tarehe 01.04.2017 alitoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza.

Kamanda Masejo ametoa onyo kali kwa baadhi ya watu wachache wenye nia ya kufanya uhalifu ama kuzuia watendaji wanaotekeleza majukum yao kuwa  Jeshi la Polisi lipo imara na litawachukulia hatua kali za kisheria na amewaomba wananchi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa nia ya kutokomeza uhalifu katika  Mkoa huo.

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2