DC Babati atangaza Vita kwa wezi wa Miundombinu ya TANESCO. | Tarimo Blog

Na John Walter-Babati

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange,ametangaza vita dhidi ya waharifu na watu wanaojihusisha na wizi wa miundombinu ya umeme na miradi ya kimkakati inayotekelezwa yenye lengo la kuchochea kukua kwa uchumi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Ametoa kauli hiyo wakati akiongea na wakazi wa Mtaa wa Komoto kata ya Bagara mjini Babati kufuatia watu wasiofahamika kufanya uharibifu na kuiba chuma katika nguzo kubwa za umeme zinazotoka nchini Tanzania hadi Kenya na kusababisha hasara kubwa kwa Tanesco.

Twange amesema Serikali haitakuwa na huruma kwa mtu au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu hasa kwenye miundombinu ambayo inajengwa kwa fedha nyingi za walipa kodi.Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya Lazaro Twange Mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 500 za Kitanzania.

Amesema, umeme ni nishati muhimu kwa uchumi wa nchi,kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi na kulinda miundombinu hiyo inayojengwa kwa lengo la kuchochea na kuharakisha maendeleo.

Mkuu wa wilaya, amewataka viongozi na wananchi katika mtaa wa Komoto na meneo yote ambayo nguzo hizo zimepita kutoa taarifa na kuwafichua watu wanaojihusisha na matukio ya wizi wa miundombinu hiyo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Twange ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama,amewaomba watendaji wa wa Serikali ngazi mbalimbali ,wenyeviti wa mitaa na Vijiji kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma maendeleo.

Kwa upande wake afisa Usalama wa wa shirika la umeme (TANESCO) mkoa wa Singida Davis Mkwiche ameeleza kuwa nguzo tisa katika wilaya ya Babati zimeharibiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi ambapo wamekata chuma ndogo zilizowekwa kuzunguka nguzo hizo.

Mradi huo wa kimkakati wa utengezaji wa njia ya kusafirisha umeme wa Kilovoti 400 unaotekelezwa kutoka Tanzania hadi nchini Kenya upo katika hatua za mwisho za kukamilika kabla ya kukabidhiwa kwa Tanesco

Mkwiche amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watu hao baada ya kuiba vyuma huvitumia kutengeneza mikokoteni ambayo inakokotwa na wanyama,mikuki na visu,bangili huku wengine wakiviuza kwa wanaoununua chuma chakavu.

Aidha Shirika hilo limeahidi zawadi nono kwa mwananchi atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa waharibifu na wezi wa miundombinu hiyo na kuwafichia siri watoa taarifa.Amesema,serikali imekuwa ikijitihadi sana kuboresha miundombinu yake,hata hivyo baadhi ya watu wachache wanarudisha nyuma juhudi hizo kwa kuharibu kwa makusudi miundombinu ya umeme na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Ameiomba jamii kushirikiana na Tanesco kulinda na kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme kwani nishati hiyo ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa.

Afisa Upelelezi kutoka jeshi la Polisi wilaya ya Babati Said Ramadhani amesema kosa la kuharibu au kuiba miundombinu ya Tanesco ni Uhujumu Uchumi ambapo adhabu yake ni kifungo na usafiri uliotumika katika uhalifu huo hutaifishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na 2019.


 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2