HAJI MANARA NAJUA HUNIJUI LAKINI NIKWAMBIE UKWELI UMEZINGUA SANA | Tarimo Blog

Na Baba Faisal

KABLA ya kwenda mbali niseme mapema Haji Manara umezingua sana na binafsi nimeshindwa kukaa kimya, acha niseme.

Unajua nini, Haji Manara ameibuka na hoja za kamba Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez anamuonea sana, eti anamchukia na imefika hatua hata akiwekewa chakula mbele yake hawezi kula.Kha! Haji bwana.

Hakuishia hapo Haji ameeleza mengii na yote akiwaaminisha wana Simba na mashabiki wa Soka la Tanzania kwamba kwa mambo anayofanyiwa ndani ya Simba yamemfika mwisho na hawezi kuendelea tena kuwa msemaji wao kwani anahofia hata usalama maisha yake.

Haji Manara najua binafsi hunijui kabsa,lakini naomba nikwambie kitendo chako cha kujirekodi na kisha kutumia sauti yako ya kumshambulia Mtendaji Mkuu wa Simba , umekosea sana.

Sijui umeshauriwa na nani na kama umetumia akili yako nikwambie safari hii akili imeshindwa kukusaidia, imekupotosha na mbaya zaidi imeamua kukugombanisha na watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikuamini,wakikupenda na kukuheshimu.Ndio ujue hivyo.

Mwanzoni niliona malalamiko ya Manara kupitia ukurasa wake kwenye mitandao ya kijamii.Swali la kwanza kunijia kichwani,hii habari ni kweli? Haji huyu ambaye tunamfahamu anaweza kuandika hiki ambacho amekiandika.Kama kawaida ya mitandao taarifa ya Manara ikaanza kusambaa kama upepo uvumao kwa kasi ,tena kasi haswaa.

Mijadala ikaanza  mitandaoni, watani wao wa jadi ( YANGA) nao wakaona nafasi ndio hiyo, na sio watani tu hata mashabiki wa soka nao wakaingia kwenye kujadili ishu hiyo.Lakini hata ingekuwa wewe jambo limeewekwa mtandaoni unakaaje kimya.Thubutu yake.

Nikiri sijui dhamira ya Haji Manara ni ipi ? Ndio sijui na tunasubiri kwa hamu atakuja na hoja gani.Lakini kibaya zaidi licha ya kuandika kwenye ukurasa wake akaona kama vile haitoshi na ujumbe wake haujafika akaamua kurekodi na sauti akaitupia mtandani,tuisikilize.Na masikio hayana pazia.Baadaye akatuma sauti nyingine, katika sauti hiyo Haji ameamua kujirekodi huku akiwa analia.Sanaa juu ya sanaa.

Swali langu la msingi kipi ambacho kimemfanya ajirekodi akiwa analia? Anataka huruma ya mashabiki wa soka? Au anataka huruma ya Mohamed Dewj a.k.a tajiri MO? Au anataka huruma ya wana Simba? Tunasubiri tutapata majibu.

Katika maisha kuna njia nyingi za kushughulika kutafuta ufumbuzi wa changamoto inayokukabili, njia nzuri ni ile ambayo utaitumia kutatua changamoto akili ikiwa na utulivu.Kwa kilichotokea kwa  Haji Manara alikosa utulivu na ukweli amekurupuka,kwa lugha ya kimjini mjini Haji amezingua sana.Acha tumwambie ukweli.

Tufanye hivi Haji Manara kweli anaonewa na Barbara pale Simba, tufanye kweli anachukiwa,tufanye kweli analipwa mshahara kiduchu huo wa laki saba.Lakini swali kutuma sauti mtandaoni ndio suluhu ya kutafuta ufumbuzi? Ndio maana nasema amezingua.

Nikiri Haji anayo nguvu kubwa huko mitandaoni,anajua kucheza na akili za watu, amekuwa mkubwa tena mkubwa haswaa,ukitaka kumuingia Haji uwe umejipanga.Ndio na wote tunafahamu.Kwa mazingira ya aina hiyo Haji amekuwa hana wa kumwambia ukweli.

Kama wachambuzi na watangazaji maarufu wa habari za michezo wanaweza kuitwa taka taka na wakakaa kimya,wewe mwingine nani uthubutu kunyanyua mdomo.

Muulize kilichomtokea Prisca Kishamba yule Mtangazaji wa Clouds, aliionja joto ya jiwe.

Manara alimbwatukia mbele ya waandishi waliokuwepo kwenye mkutano ambao pia ulikuwa Live kwenye vyombo mbalimbali vya habari.Binafsi nilijisikia vibaya lakini ukisema jiandae kusemwa na Manara.

Kibaya zaidi wakati anafanya hayo yote uongozi wa Klabu ya Simba umekuwa kimya na matokeo yake Haji ametengeneza sayari yake ya kuishi, ataamua kusema na kufanya anachotoka.

Akaona sasa amekuwa mkubwa na kuna wakati nadhani anahisi Simba bila yeye haitafanya lolote.

Kama anafikiria hivyo anajidanganya.Ndio ajue sasa.

Historia ya Simba hata Yanga tunazifahamu, ni vilabu vikongwe sana katika soka la Tanzania na Afrika Mashariki, na ukongwe huo umefanya Simba watu wengi wapite na kutoa mchango wao kuhakikisha klabu inasonga mbele.Hivyo hata Haji atapita Simba na Simba itabaki kwa mazingira yoyote il yawe mazuri au mabaya.

Kilichonisikitisha zaidi ni pale Haji anapoamua kuibua matatizo yake wakati akijua siku mbili au tatu kuna mechi ngumu kati ya timu yake ya Simba na Yanga, tena ni fainali ya Kombe la Shirikisho inayofanyika Kigoma Julai 25.

Swali lengo la Haji Manara ni lipi? Anataka kuisaidia Simba ishinde au anataka kuisaidia Yanga? Anatoa tuhuma nzito kwa Mtendaji Mkuu wa Simba akijua kuna mechi ya watani wa wa jadi je anataka kumtoa Barbara na Wana Simba kwenye malengo ya kushinda mechi hiyo.

Tunaweza kuamini kweli kuwa hajawahi kuihujumu Simba Klabu ya Maisha yake kama ambavyo anasema lakini kitendo cha kuanzisha chokochoko na Klabu tena siku chache kuelekea fainali ya FA dhidi ya Yanga ni hujuma kubwa kuliko ya kuchukua fedha.

Ambacho Manara hajui ni kwamba hao ambao wanampatia mikataba mikubwa wamekua wanampatia kwa sababu ya brand kubwa aliyonayo ambayo bila shaka ameipata kwa nafasi yake ya Usemaji wa Simba.

Kama yeye mwenyewe amewahi kukiri kuwa hakuna Taasisi kubwa na imara Afrika Mashariki zaidi ya Simba je ni wapi ataenda ambapo patampa nafasi kubwa zaidi ya hapo alipo?

Kusema Barbra anamuonea hatuwezi kukataa lakini kitendo chake cha kutuma voice note akimfokea Boss wake ni kuonesha dhahiri yeye hana nidhamu kwa viongozi wake.

Huwezi kubishana na Boss wako kama unabishana na mtoto mdogo au shabiki. Ule ni ukosefu wa nidhamu, kiburi na majivuno.

Manara umeikosea Klabu yako, umewakosea Mashabiki wa Simba waliokuamini kwa muda mrefu na zaidi umenikosea hata wewe mwenyewe kwa kuonesha jinsi gani upande wako wa pili ulivyo.

Anasema anaipenda sana Simba,ndio anaipenda lakini kwa alichokifanya ameonesha kutoipenda Simba bali anapenda maslahi anayoyapata kupitia Simba.Haji nikwambie ukweli umezingua broo.Kumbuka anayekwambia ukweli anakupenda.Alamsiki.


 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2