MAFIA WASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA PASS KUKUZA BIASHARA ZAO. | Tarimo Blog

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya PASS Trust, Anna Shanalingigwa akizungumza Wadau wa kilimo, uvuvi na ufugaji wilayani Mafia katika warsha ya siku mja iliyofanyika jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Martin Mtemo ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza katika warsha hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia,Martin Mtemo (katikati) akiwa na timu ya Wafanyakazi wa PASS walipotembelea Kiwanda cha Usamabazaji Samaki cha Mkaire General Supplies kinacho milikiwa na  Ismail Kamugisha Mkazi wa Mafia ambaye amekiboresha baada ya kuwezeshwa na PASS.


Na Mwandishi Wetu, Mafia

WADAU wa kilimo, uvuvi na ufugaji wilayani Mafia wameaswa kutumia fursa ya Upatikanaji wa mikopo ya fedha na zana za kisasa za kutendea kazi zao kupitia huduma zinazowezeshwa na Taasisi ya PASS TRUST ikishirikiana na Kampuni tanzu yake ya PASS LEASING.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Martin Mtemo alipokuwa akizungumza na wadau hao walipokutana katika warsha maalumu ya wiki ya PASS iliyoandaliwa na Kampuni hiyo wilyani humo ambapo pamoja na mambo mengine, Mtemo amewaasa wakulima, wafugaji na wavuvi hao kuunda vikundi ili waweze kunufaika na fursa zinazotolewa na Kampuni hizo pacha.

“Wilaya yetu ya Mafia imebarikiwa kwa kuwa na fursa nyingi katika uvuvi na kilimo, na kama mnavyojua changamoto kubwa ambayo imekuwa ikifanya shughuli hizi ziwe za kusuasua ni ukosefu wa mitaji, Sasa kwa kushirikiana na PASS nawaasa wakulima na wavuvi chukieni hizo pesa muwekeze katika uvuvi na kilimo” alisema mkuu huyo wa wilaya huku akiwatoa hofu wadau hao kuhusu dhana potofu inayopelekea hofu miongoni mwa watanzania katika kuchukua mikopo benki kwa ajili ya kukuza biashara zao.

“Serikali inatambua mchango wa PASS katika kuendeleza shughuli za kilimo nchini, hapo mwanzo wakulima wengi walikuwa hawakopesheki kwa kukosa 

dhamana lakini PASS ni Taasisi ambayo imeanzishwa hapa nchini mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kukopesheka katika benki zetu, kwahakika hii ni fursa muhimu sana kwetu na niombe wanamafia msiogope serikali ipo na tunafanya kazi kwa ushirikiano na PASS, kopeni mfanye kazi ili tupate maendeleo” alisema Mtemo.

Kufuatia ufafanuzi wa kina juu ya huduma za kampuni hizo ambapo Meneja wa Kanda ya Mashariki, Hadijali Seif aliwaeleza wadau wa mkutano huo kuwa PASS Trust inawezesha udhamini wa mikopo ya fedha kwa wajasiriamali wa kilimo biashara kuanzia 20% hadi 60% kwa kinababa na 20% hadi 80% kwa vijana na kinamama na baadaye Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa PASS, Hamis Mmomi akafafanua kuwa Kampuni tanzu ya PASS Leasing yenyewe inajikita na ukodishaji wa zana za kutendea kazi katika mnyororo mzima wa kilimo, uvuvi na ufugaji bila dhamana yoyote, wadau hao walieleza kufurahia huduma hiyo na kuomba PASS kuongeza uwekesaji katika wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuwatembelea mara kwa mara ili wakulima wengi waweze kufikiwa na huduma hiyo.

Miongoni mwa wadau waliotoa maoni yao juu ya huduma za PASS Trust na Kampuni tanzu yake ya PASS Leasing ni Afisa Uvuvi wa wilaya hiyo ya Mafia Anthony Mbega ambaye alidokeza kuwa PASS imekuja kuwa suluhisho kwa wakulima wa wilaya hiyo kwa kujaza nafasi ambayo inaachwa wazi kutokana na bajeti ya halmashauri kutotosheleza mahitaji ya mikopo kwa wajasiriamali.

“Kwa niaba ya wavuvi nashukuru Sana taasisi ya PASS kwa kutuletea fursa hii adimu kwani hapo awali wavuvi wetu wamekuwa wakikosa mikopo kutokana na ufinyu wa bajeti ya halmashauri yetu. Sasa kwakuwa samaki tunao, wavuvi wapo na Sasa PASS wekuja naomba wavuvi na wakula wote na wavuvi undeni vikundi vya ushirika ili kuweza kunufaika zaidi na fursa hii ambayo wawezeshaji hawa wametuletea hapa” aliwaasa Mbega na kuongeza kuwa serikali wilayani humo itahakikisha inafanya kazi kwa karibu na wajasiriamali wote watakaohitaji mikopo ya fedha na zana za kilimo ili kuwawezeha kupata huduma hiyo kiurahisi.

Wakitoa shuhuda jinsi walivyoongeza thamani katika biashara zao, baadhi ya wanufaika wa huduma za PASS walibainisha kuwa udhamini wa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi unaofanywa na Kampuni hiyo umewasaidia kukuza uwekesaji wao na kuzalisha ajira katika Biashara zao za uvuvi na kilimo.

“Sehenmu kubwa ya uwezekaji wangu ambao naufanya katika uvuvi wa meli nimeupata kutokana na udhamini wa PASS ambao walinidhamini nikapata mkopo wa milioni 75 kutoka benki, nikawekeza na ndiyo imenifanya nifikie hatua hii kama mnavyoniona, kwakweli nawashukuru PASS” alisema, Said Issa Kombo mkazi wa Kisiwani Mafia.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya usindikaji na usamabazaji samaki, Mkaire General Supplies, Ismail Kamugisha aliweka wazi kuwa mafanikio yake hadi kuimarisha kampuni hiyo yametokana na mkopo aliowezeshwa na PASS kutoka benki ambapo bila udhamini wa PASS asingekopesheka kutokana na taratibu za kibenki.

“Kwakweli Kampuni ya PASS imenisaidia sana kukuza uwekezaji katika biashara yangu kwani hapo awali nilikuwa nasindika tani 5 kwa siku lakini tangu miaka miwili iliyopita baada ya PASS kuniwezesha kupata mkopo ninasindika hadi tani 800 kwa masaa 22. PASS walinidhamini 75% ya mtaji ambapo nilitumia 25% tu.

ya gharama za kuweza kumiliki mitambo hii ya usindikaji wa samaki” alieleza Mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa kwasasa biashara yake ni kubwa kiasi kwamba pamoja na kuwa msambazaji mashuhuri wa samaki Wilaya ya Mafia pia anasafirisha samaki wa kutosha kwenda katika masoko ya Dar es Salaam.

Maadhimisho ya wiki ya PASS Trust pamoja na PASS Leasing yenye kauli mbiu ya Pamoja tuwezeshe Upatikanaji wa fedha kwa kilimo endelevu yamefanyika wilayani Mafia ikiwa ni Mwendelezo wa maonesho hayo tangu yalipoanza mwanzao Julai 19 mwaka huu mkoani Singida na baadaye Dodoma huku baada ya Mafia kilele chake kikiwa katika Visiwa vya Zanzibar ambapo lengo kuu la Maadhimisho hayo kama ilivyoelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni  ya PASS Anna Shanalingigwa ni kuweza kupata mrejesho kutoka kwa wanufaika wa huduma zake, kuwakutanisha wadau wa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ili kujadili changamoto zilizopo na jinsi ya kuzitatua kwa na kutoa elimu na taarifa juu ya huduma za kampuni hiyo ya PASS Trust pamoja na Kampuni tanzu yake mpya ya PASS Leasing ili kuweza kuwapata na kuwasaidia wateja wapya wenye uhitaji wa huduma hizo.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2