Dk Mpango alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la Maonyesho ya benki hiyo lililopo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ‘Sabasaba’ yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema ipo haja kwa taasisi za kifedha nchini kukaa na wadau hususani wa sekta binafsi ili kuona namna ya kuwasaidia ikiwemo kuangalia suala zima la riba zinazotozwa na benki hizo ili wafanyabiashara wengi zaidi waweze kufaidika na mikopo hiyo kwa kukuza mitaji yao.
“Udhamini mkubwa wa Benki ya NBC katika maonesho haya unaweza kuwa ishara njema katika kuonesha namna gani inaguswa na inahitaji kuwa karibu na wafanyabiashara naomba sana muendelee kuwa karibu nao ili muwasaidie nanyi pia muendelee kuboresha huduma zenu,’’ alisema Dk Mpango
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alisema ushiriki na udhamini wa benki hiyo katika maonesho hayo kwa kiasi kikubwa unachagizwa na namna benki hiyo inavyohitaji kuwa karibu na wadau wake hususani wafanyabiashara.
“Uwepo wetu kwenye maonesho haya haujaishia tu kwenye kuonesha na kutoa huduma zetu bali umeenda mbali zaidi kwa kuhakikisha kwamba tunashirikiana na waandaaji yaani Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ili kuona kwamba wadau wetu pia wakiwemo wajasiriamali si wanashiriki wanashiriki bali pia wanashiriki katika mazingira mazuri zaidi chini ya mwamvuli wa NBC,’’ alisema.
Hivi karibuni Benki hiyo iliingia makubaliano maalum na TanTrade yanayohusisha ufadhili wa benki hiyo katika ujenzi na ukarabati wa kumbi kubwa za kisasa kwenye viwanja vya Maonesho hayo sambamba na ujenzi wa sanamu ya Rais wa Awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli.
Wakizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini hati ya makubaliano (MoU) yenye jumla ya thamani ya Tsh mil 420 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Balozi Mteule Edwin Rutageruka pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi walisema hatua hiyo inalenga kuleta mapinduzi makubwa kwenye Maonesho hayo yanayoendelea jijini humo huku yakivutia maelfu ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.
“Haya yote yanadhihirisha namna benki ya NBC inavyoshiriki katika kuchochea mazingira bora ya ufanyaji biashara,’’ alisema Balozi Mteule Rutagaruka huku akitolea mfano wa uwepo wa Kliniki ya biashara inayofadhiliwa na benki katika maonesho hayo ikihusisha uwepo wa taasisi na mamlaka mbalimbali za kibiashara ikiwemo Tantrade, Shirika la Viwango nchini(TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi akiwa ameshikilia tuzo ya kikombe maalum kutoka kwa waandaaji wa Maonyesho ya Kimataifa ya biashara ya Sabasaba, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo kama mdhamini mkuu wa maonesho hayo.
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango (kushoto) akizungumza na viongozi waandamizi wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi (wa pili kulia), Meneja Mahusiano wa Benki hiyo Bw William Kallaghe (kulia) pamoja Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Balozi Mteule Edwin Rutageruka ( watatu kulia) wakati Makamu wa Rais alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi akizungumza mbele ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango (Hayupo pichani)pamoja na viongozi waandamizi wengine wa serikali, pamoja na washiriki mbalimbali kuhusu ushiriki wa benki hiyo kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Benki ya NBC ndio mdhamini mkuu wa Maonesho hayo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof Kitila Mkumbo (Kushoto) akiangalia kumbukumbu ya vitu vya kale vilivyotumiwa na benki ya NBC alipotembelea banda la Maonyesho la benki hiyo lililopo kwenye uwanja wa Maonyesho ya Kimataifa ya biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi waliotembelea Maonyesho ya Kimataifa ya biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam wakitazama moja ya gari lililokuwa likitumiwa na viongozi waandamizi wa benki ya NBC miaka iliyopita. Gari hilo lipo mbele ya banda la benki hiyo kwenye uwanja wa maonesho hayo.
Huduma za benki ya NBC zikiendelea kutolewa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye Maonyesho hayo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment