Changamoto ya urasimiswhaji wa biashara miongoni mwa wajasiriamali na wafanyabiashara wanaochipukia imetajwa kuwa moja ya kikwazo kikubwa kwa wao kuendesha shughuli zao kwa ushindani na hivyo kukosa ukuaji endelevu.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Benki ya NBC kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na taasisi nyingine 15 zimeweka kambi kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya jijini Dares Salaam ‘Sabasaba’ ili kuwasaidia wafanyabiashara hao.
Akizungumza kwenye maonesho hayo mwishoni mwa wiki, Afisa Habari Biashara kutoka TANTRADE Bi, Miriamu Kikoti alisema kupitia Kliniki ya Biashara inayosimamiwa na TANTRADE na kudhaminiwa na Benki ya NBC wameweza kuwakutanisha wataalamu wa Biashara kutoka Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi ambao hushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wajasirimali na Wafanyabiashara nchini ikiwemo suala zima la urasimishwaji biashara.
Mbali na TANTRADE na Benki ya NBC, Bi Kikoti alizitaja taasisi nyingine zinazoshiriki kikamilifu kufanikisha mkakati huo wa pamoja kuwa ni pamoja na EPZA, BRELA, TIC, GS1, TRA, WMA, TBS, SIDO, FFC,UDSM,TIRA,TFS, GCLA, FCC, TMDA na OSHA.
“Changamoto kubwa kwao ni urasimishwaji wa biashara zao. Hadi kufikia sasa mbali na kutoa huduma za ushauri kwa mamia ya wajasiriamali na wafanyabiashara wanaochipukia wanaotutembelea kila siku tangu maonesho haya yaanze, tumefanikiwa kuwasaidia wajasiliamali zaidi ya 120 kuelekea katika urasimishwaji wa biashara zao.’’
“Hili tunalifanya kwa urahisi sana kwasababu kupitia kliniki hii wahusika wanapata cheni iliyokamilika na hivyo wanaondoka wakiwa wamekalimisha kila kinachohitajika,’’ alifafanua.
Aliishukuru benki ya NBC kwa uamuzi wake wa kudhamini Kliniki hiyo kwa kuwa mkakati huo mbali na kuwasaidia wajasiriamali hao, kwa kiasi kikubwa pia umekuwa ukifungua njia kwa taasisi za kifedha kutoa huduma za mikopo kwa wajasiriamali ambao wana sifa za kukopesheka kutokana na kuendesha shughuli zao kwa urasmi unaotakiwa na taasisi hizo huku pia wakiwa na uhakika wa kufanya marejesho ya mikopo.
Mafanikio ya Kliniki hiyo yalidhihirishwa Oktoba 14, 2020 ambapo ilitajwa kuwa mshindi wa tatu wa dunia (Best use of partnership category) na wa pekee kutoka nchi za Afrika kwenye Tuzo za Taasisi zinazosimamia Biashara duniani (WTPO Awards 2020)
Kwa upande wake Mkuu wa Chapa na Mawasiliano kutoka NBC, David Raymond alisema kwa kutambua umuhimu wa urasimishwaji biashara mingoni mwa wajasiriamali na wafanyabiashara wanaochipukia nchini benki hiyo haikusita kufadhili kliniki hiyo ili kuyaandaa makundi hayo yaweze kupata vigezo vitakayoyawesha kupata huduma mbalimbali za benki hiyo ikiwemo mikopo.
“Benki ya NBC tumeendelea kuwa karibu na wafanyabiashara wa kati (SMEs) na ndio maana tumezidi kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji yao kama vile mikopo ya bila dhamana kwa wazabuni na wasambazaji wa bidhaa, huduma za kidigitali zinazookoa muda pamoja na gharama nafuu zaidi za uendeshaji ili kuongeza tija kwenye biashara zao,’’ alisema.
Alitolea mfano akaunti ya ‘NBC Kua Nasi’ inayowalenga wafanyabiashara wanaochipukia wakiwemo mama lishe, madereva bodaboda,wasindikaji, wasusi pamoja na makundi mengine kwa kuwawezesha kutunza pesa zao kwa usalama na urahisi zaidi bila gharama za uendeshaji.
Afisa Habari Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE)Bi, Miriamu Kikoti (katikati) akimsikiliza mmoja wa wajasiriamali (Kulia)aliefika kwenye banda la Kliniki ya Biashara inayosimamiwa na TANTRADE kwa ufadhili wa Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya jijini Dares Salaam ‘Sabasaba’. Kliniki hiyo imewakutanisha wataalamu wa Biashara kutoka Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi ambao hushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wajasirimali na Wafanyabiashara nchini ikiwemo suala zima la urasimishwaji biashara.
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakitembelea kwenye banda la Kliniki ya Biashara inayosimamiwa na TANTRADE kwa ufadhili wa Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya jijini Dares Salaam ‘Sabasaba’.
Wajasiriamali na wafanyabiashara wanaochipukia wakipata huduma za kibiashara walipotembelea kwenye banda la Kliniki ya Biashara inayosimamiwa na TANTRADE kwa ufadhili wa Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya jijini Dares Salaam ‘Sabasaba’.
Maofisa kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo EPZA, BRELA, TIC, GS1, TRA, WMA, TBS, SIDO, FFC,UDSM,TIRA,TFS, GCLA, FCC, TMDA na OSHA wakitoa huduma zao kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wanaochipukia waliotembelea kwenye banda la Kliniki ya Biashara inayosimamiwa na TANTRADE kwa ufadhili wa Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya jijini Dares Salaam ‘Sabasaba’.
Pamoja na huduma za kibenki, washiriki wanaotembelea banda la Maonesho ya Sabasaba la Benki ya NBC wamekuwa wakipatiwa zawadi mbalimbali.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment