Adeladius Makwega -Kwimba Mwanza (WHUSM)
SERIKALI imesema kuwa Watanzania wanahitaji burudani ya muziki kwani mara baada ya kujishughulisha na shughuli za maendeleo mchana kutwa basi jioni ni muda wa kupumzisha miili na akili zao.
Hayo yamesemwa Julai 17, 2021 katika mahafali ya 10 ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ambapo Mheshimiwa Pauline Gekul Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amekuwa mgeni rasmi.
“Watanzania tunapenda muziki iwe dansi, Bongo fleva, rege au muziki wa kiutamadauni, si mmeona wanachuo cha Malya walivyokuwa wakicheza muziki vizuri, huku wakinengua? huo ndiyo muziki” alisema Mheshimiwa Gekul.
Yawe mashairi au ala za muziki zinaweza kumtoa nyoka pangoni alisema kwa bashasha huku akiiweka vizuri mikrofoni wakati wa mahafali hayo.
Tanzania yetu ina utajiri mkubwa wa muziki mathalani nyimbo za zamani zimekuwa zikipigwa katika baadhi ya redio na kumbi za starehe. Serikali chini ya Jemedari, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inatoa ushirikiano wa kutosha kwa wanamuziki wa Tanzania.
Pia aliikumbusha hadhira wakati wa mahafali hiyo kuwa muziki wa Kitanzania unamchango katika kukikuza Kiswahili, tunawapenda wanamuziki wetu na ndiyo maana Serikali katika Bajeti ya sasa 2021/2022 imeweka bilioni 1.5 katika kukuza Sanaa nchini.
Akiunga mkono kauli hiyo ya Serikali Samsoni Mhando ambaye ni mdau wa muziki hasa wa zamani nchini amesema kuwa ni kweli muziki wa Tanzania unapendwa sana na umekikuza mno kiswahili lakini zipo changamoto za hapa na pale.
Mdau huyu ambaye alikuja kwenye mahafali ya mtoto wake aliyehitimu mafunzo hayo Stashahada ya Michezo anaamini kuwa Serikali imeshaanza kuzitatua changamoto zote za muziki ikiwamo suala la mirabaha ambalo ni mwazo mwema.
“Mimi nampenda sana Mbaraka Mwinshekhe na nazipenda mno nyimbo zake, hakuna siku inayonipita bila ya kusikiliza wimbo wa Mbaraka kwani ndani yake nimekuwa nikipata elimu na burudani” anasema ndugu Mhando.
Mdau huyo wa muziki anakubaliana na kauli ya Serikaili juu ya upenzi wa Watanzania katika muziki na ndiyo maana baadhi ya wanamuziki wa zamani wamefariki lakini nyimbo zao bado zinaishi na zinapendwa.
Akitaja baadhi ya wanamuziki waliofariki; Mbaraka Mwinshekhe (Mtaa wa Saba), Marijani Rajabu (Mayasa), Salim Abdalla (Mkono wa idd), Moshi William (Ndoa ndoano), Muhidini Ngurumo (ikiwa kam haunitaki), Shabani Dede (Fatuma), Shem Kalenga (dada Asha) na wengine wengi wanaendelea kukonga nyoyo za Watanzania.
“Kilichokuzuzua ni nini, mwenyewe ukanirudia tena, Je umepambana na nini dada huko ulipokwenda, Maisha uliyopata kwangu dada oh oh, Hautapata kwa mwingine dada oh oh, Kaa sasa utilie ewe dada oh oh.”
Mdau huyu alidokeza kwa kuimba sehemu ya wimbo huo alinainisha kuwa unafahamika kama "Kilichokuzuzua ni nini?" kutoka kwa bendi ya Morogoro Jazz iliyoongozwa na Mbaraka Mwinshehe.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment