Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa Singida Dkt.Binilith Mahenge amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia ujio wa Taasisi ya mikopo ya Pass inayojishughulisha na utoaji wa mikopo na udhamini kwa wakulima kama fursa kwao katika kilimo cha alizeti.
Dkt. Mahenge aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akifungua mkutano wa wadau wa kilimo cha zao la alizeti ulioandaliwa na taasisi hiyo.
"Nawahasa wananchi wangu wa Singida muichukulie taasisi ya Pass kuwa ni fursa moja wapo itakayowawezesha kuharakisha kuwaletea maendeleo," alisema Mahenge.
Alisema Serikali mkoani hapa itawapa Pass ushirikiano wa kutosha ili wananchi wapate huduma hizo muhimu zitakazo wainua kiuchumi kupitia kilimo cha alizeti.
Mahenge aliitaka taasisi hiyo kupanua wigo wa kujenga uelewa kwa kufanya mikutano mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya jambo litakalosaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma bora kwa kutumia fursa ya uwepo wa Taasisi hiyo na mabenki kwa ufanisi zaidi.
Pia alisema itawezesha kutengeneza mazingira mazuri ya kuibua changamoto nyingi na kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kukabiliana nazo ili kuyafikia mapinduzi ya kilimo.
Alisema wakulima wengi ni wadogo na bado wanatumia teknolojia duni lakini kupitia taasisi kama hiyo wataweza kuweka mazingira rafiki ya kuwafikia wadau wengi wa sekta ya kilimo kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa haliwezi kuzifikia taasisi za kifedha kwa ufanisi.
Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Taasisi hiyo Hamisi Mmomi akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Taasisi hiyo alisema tangu taasisi hiyo ianzishwe hadi kufikia mwezi Desemba mwaka jana tayari wamekwisha wakopesha wakopaji zaidi ya 46,000 na kudhamini mikopo ya Trioni 1.08.
Alisema katika wakopaji hao 46,000 wanufaika wa moja kwa moja ni zaidi ya milioni 1.6 kwa sababu wakopaji wengine kama vyama vya ushirika kuna wanachama kuanzia 50, 100 hadi 200 hivyo kufikisha idadi hiyo.
Alisema mikopo hiyo imetengeneza ajira zaidi ya milioni 2.5 kutokana na wakulima kuajiri wakulima na kuwa mikopo hiyo wakopaji wamekuwa wakiirejesha kwa wakati kutokana na utaratibu mzuri waliouweka wa kuipitia miradi walioikopea fedha hizo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment