Serikali inatarajia kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 170 kujenga vituo vinne vya umahiri katika mikoa minne nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati alipotembelea Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza ambapo amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 37 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umahiri wa sekta ya ngozi katika kampasi hiyo.
"Tunataka ifikapo mwaka 2024 tuwe tumekamilisha ujenzi wa Kituo cha umahiri katika masuala ya ngozi, ili sasa tuweze kuzalisha vijana ambao wakimaliza mafunzo yao waweze kuajiriwa au kujiajiri," amesisitiza Kipanga.
Kipanga ametaja vituo vingine vya umahiri vitakavyojengwa kuwa ni Kituo cha umahiri wa sekta ya anga ambacho kitajengwa katika Chuo cha Usafirishaji (NIT) Jijini Dar es Salaam, kituo cha umahiri wa TEHAMA kitakachojengwa DIT kampasi ya Dar es Salaam na kituo cha umahiri wa nishati jadidifu kitakachojengwa DIT kampasi ya Arusha.
"Kimsingi Serikali imeamua kwa dhati kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi na umahiri ambao utaleta tija kwenye Tanzania ya viwanda hivyo inakwenda kujenga vituo vinne vya umahiri hadi kufikia mwaka 2024," amesema Naibu Waziri Kipanga.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa DIT, Profesa Praxedius Ndomba amesema kampasi ya Mwanza inajihusisha na mafunzo, utafiti na uzalishaji wa bidhaa za ngozi ikiwemo viatu, mikanda, mabegi na mipira ya kuchezea.
Aidha ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha vituo vya umahiri ambavyo anaamini vitakwenda kuboresha elimu ya mafunzo ya ufundi nchini kwa kiwango kikubwa.
Awali akisoma taarifa ya kampasi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Issa Mwangosi amesema mwaka 2010 hadi 2020 wametoa wahitimu 1,339 wa kozi za muda mfupi na wahitimu 29 wa kozi za muda mrefu za Stashahada mwaka 2018 hadi 2020.
Amesema kampasi hiyo kwa sasa inatoa kozi za fani ya utengenezaji bidhaa za ngozi, sayansi na teknolojia ya maabara; na TEHAMA, zote katika ngazi ya Astashahada na Stashahada.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (katikati, waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo kampasi ya Mwanza.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza na watumishi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wakati alipotembelea kampasi ya Chuo hicho iliyopo Mwanza.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment