Na Redempta Ndubuja - MAELEZO
SERIKALI inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inatekeleza kwa kasi miradi mbalimbali iliyoachwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa katika mahojiano maalum na chaneli moja ya televisheni iliyopo nchini.
“Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) umefikia asilimia 92 na mwezi Novemba treni ya majaribio itatoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro na kutoka Morogoro kwenda Singida ambapo ujenzi katika kipande hiki umefikia asilimia 65.
“Kuhusu kipande cha kutoka Mwanza hadi Isaka fedha za awali shilingi bilioni 372 tayari imeshatolewa na kazi inaendelea, Rais Samia ameshaliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuanza maandalizi ya kutafuta wakandarasi wa kuanza kujenga kutoka Makutupora - Tabora - Isaka - Kigoma - Kaliua - Mpanda- Kalema,” amesema Msemaji Mkuu wa Serikali.
Pamoja na hilo, Msigwa amesema utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umefikia zaidi ya asilimia 53 na ifikapo mwezi Juni mwaka 2022 utaanza kutoa umeme na kwamba Serikali tayari imeshatoa shilingi tilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, amefahamisha kuwa mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigongo - Busisi utakaogharimu takriban shilingi bilioni 700 umefikia asilimia 27 na kwamba Mhe. Rais Samia ametoa maagizo mradi huo ukamilike ndani ya muda.
Sambamba na hayo, Msigwa ameeleza kwamba kwa mwaka 2021/2022, Serikali imejipanga kutekeleza miradi 315 ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 86 vijijini ambapo miradi 114 yenye thamani shilingi bilioni 317 itatekelezwa mijini.
“Tunategemea kupeleka shilingi bilioni moja katika kila jimbo kwa ajili ya barabara, tuna tatizo kubwa la barabara vijijini ndio maana Serikali inataka ianze safari ya ujenzi wa barabara hizo,” amedokeza.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment