SERIKALI YATENGA ZAIDI YA SH BILIONI MOJA KWA AJILI YA UJENZI WA MAJENGO YA TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI | Tarimo Blog

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kukamilisha ujenzi wa majengo katika Taasisi ya Sayansi za Bahari  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Buyu, Zanzibar

Akizungumza baada ya kukagua chuo hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amesema Wizara kupitia mradi wa kuendeleza Elimu ya Juu tayari imeshatenga zaidi ya Sh Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Taasisi hiyo.

Waziri Ndalichako amesema mbali ya fedha hizo Wizara imeshaanza kufanya mapitio ya miradi yake ili kuona namna ya kupata fedha za kumalizia ujenzi wa majengo ambayo tayari misingi yake imeshajengwa na imekaa muda mrefu bila kukamilishwa.

"Mbali ya kutenga fedha za ujenzi wa mabweni, lakini mimi na Katibu Mkuu tulishaanza kufanya mapitio  miradi tuliyonayo katika wizara kuona inawezaje kusaidia kukamilisha ujenzi wa majengo yote yaliyoishia katika hatua ya msingi ambayo ni muhimu katika kukamilisha mafunzo," Amesema Prof Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema kamwe Serikali haiwezi kuona fedha zilizotumika kujenga misingi hiyo zinapotea bure kwa kuwa hakuna fedha za kukamilisha ujenzi.

Amesema matamanio yake ni kuona majengo hayo yanaanza kujengwa katika mwaka 2021/22 na kukamilika mwaka 2022/23 ili madhumuni ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yafikiwe ikiwa pamoja na kutekeleza sera ya uchumi wa bluu.

Aidha, ameupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kuanza masomo pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali, amezisitiza kuwa chuo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  juu ya kuandaa vijana wenye ujuzi ambapo Taassisi hiyo ina Programu za  mafunzo mbalimbali ambayo yanatoa ujuzi katika tasnia ya Sayansi ya Bahari.

Naye Mbunge wa Kiembe Samaki, Zanzibar ambapo Taasisi hiyo ipo, Mohammed Maulid amemshukuru Waziri Ndalichako kwa kufika katika Taasisi hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa taifa katika kuandaa wataalamu wa sayansi ya majini ambao wataiwezesha kufanikisha uchumi wa bluu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari, Dk Magreth Kyewalyanga amemwambia waziri kuwa ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyo kwenye hatua ya msingi zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni saba  na milioni mia tano.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi DARUSO, Frank Buluma amesema Taasisi hiyo imewasaidia wao kama vijana kupata fursa  ya kupata elimu ya Sayansi  ambayo itawawezesha kushiriki katika kukuza uchumi kupitia uchumi wa bluu. Ametoa wito kwa vijana kujiunga na chuo hicho ambacho kitawawezesha kupata elimu itakayowasaidia kujiajiri katika eneo jipya la ajira.

Taasisi ya Sayansi za Bahari, inatoa mafunzo katika ngazi umahiri, uzamivu na shahada za awali,  kufanya tafiti na kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali ya Sayansi ya Bahari.

Muonekano wa moja ya majengo ya Taasisi ya Sayansi za Bahari yaliyopo Buyuni Zanzibar  yaliyokamilika kujengwa.
Mbunge wa Kiembe Samaki, Mohammed Maulid akizungumza katika kikao cha waziri na watumishi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari, wakati Waziri Ndalichako alipofanya ziara katika Taasisi hiyo Buyu, Zanzibar.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akitoa maelekezo kuhusu namna ya ukamilishaji wa miundombinu ambayo haijakamilika  kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Buyu, Zanzibar Dkt. Magreth Kyewalyanga alipotembelea Taasisi hiyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya majengo ambayo hayajakamilika na Ä·usikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Dk Magreth Kyewalyanga alipotembelea Taasisi hiyo kuona maendeleo ya ujenzi wa majengo mbalimbali.
 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2