TUTABORESHA MIUNDOMBINU YA UMEME NA BARABARA MGODI WA IMALAMATE-DC ZAKARIA | Tarimo Blog



Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema atafanyia kazi vilio vya wachimbaji wadogo katika mgodi wa Imalamate, ambao wameomba uongozi wa Wilaya ya Busega kupeleka huduma ya nishati ya umeme na kujenga barabara itakayowezesha kuboresha mazingira ya mgodi huo, hivyo kuongeza uzalishaji. Mhe. Gabriel Zakaria ameyasema hayo tarehe 26 Julai 2021 alipotembelea mgodi huo kusikiliza kero za wachimbaji wadogo.

Katika kikao hicho, Mhe. Gabriel Zakaria ameweza kusikiliza kero zilizopo katika mgodi huo, huku akisisitiza kwamba kero zilizobainishwa zitatatuliwa kwani anapenda kuona kila mchimbaji katika mgodi huo anapata haki yake. “Mimi ni mhubiri wa amani na haki, hivyo sitopenda kuona mnakosa haki yenu kwani wote mnatafuta” aliongeza Mhe. Gabriel Zakaria.

Mhe. Gabriel Zakaria amesema amesikia vilio na kero za wachimbaji wadogo, hasa kero ya kutokuepo kwa umeme wa uhakika na miundombinu mibovu ya barabara, hivyo amesema atahakikisha huduma ya nishati ya umeme inafika katika mgodi huo. “NItaongea na na TANESCO ili kufanikisha huduma ya nishati katika mgodi huo” alisema Mhe. Gabriel Zakaria. Aidha, Mhe. Gabriel Zakaria amewatoa hofu wachimbaji wadogo, na kusema kwamba anaelewa changamoto zinazowakabili wachimbaji hao ikiwemo ya kukosa huduma ya nishati ya umeme ambayo inasababisha kuwepo kwa uzalishaji mdogo na wizi hasa nyakati za usiku.

Kero nyingine zilizobainishwa na wachimbaji hao ni pamoja na tozo na kodi kubwa, kutofanyika kwa mnada kwa wakati, na matukio ya uhalifu nyakati za usiku. Akijibu Sehemu ya kero hizo Afisa Madini Mkoa wa Simiyu Mhandisi Amini Msuya amesema kuwa mchimbaji yeyote atakayepata kero au changamoto awasilishe malalamiko katika vyombo vinavyohuskia ikiwemo Ofisi ya Madini Mkoa, na malalamiko yatafanyiwa kazi kwa wakati.

Kwa Upande miwngine Mhandisi Msuya ameweza kutoa ufafanuzi wa mgawanyo wa mifuko ya mchimbaji, akisema kwamba asilimia 70 ya mifuko ni mali ya mchimbaji, wakati asilimia 20 ni ya kampuni yenye leseni na asilimia 10 ni mali ya mwenye shamba, huku akiwataka wamiliki wa leseni kutozidisha asilimia za mgawanyo wa mifuko kwani kufanya hivyo ni kukiuka utaratibu na miongozo.

Mhe. Gabriel Zakaria kwa mara ya kwanza ametembelea mgodi wa Imalamate huku akiweka dhamira ya kutatua kero za wachimbaji wadogo, ambapo mgodi huo una zaidi ya wachimbaji wadogo 5,000. Mhe. Gabriel Zakaria amesema iili kutengeneza mazingira bora ya kufanyia kazi, ni lazima malalamiko ya wachimbaji wadogo yafanyiwe kazi, lakini pia kuboresha miundombinu katika mgodi huo.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2