VODACOM TANZANIA FOUNDATION YAWAPA WATOTO NJITI FURSA KUISHI | Tarimo Blog

Ilikuwa ni asubuhi ya kawaida tu kama nyingine, siku hiyo mwaka jana ambapo Mama Hadija (siyo jina lake), ambaye ilikuwa bado wiki chache afikie siku yake ya kujifungua, alikuwa akiendelea na taratibu zake za usafi asubuhi, alipoanza kusikia uchungu usio wa kawaida. Kwa kuwa yeye mwenyewe ni mhudumu wa afya, alielewa mara moja kuwa kulikuwa na tatizo kubwa. Alikimbizwa kwenye kituo cha afya ambapo ilithibitishwa kuwa alikuwa na matatizo na hivyo kufanyiwa operesheni ya dharura na kujifungua mapacha. Mmoja kati ya hao watoto hakupona. Kwa mwingine, kwa kuwa alizaliwa wiki kadhaa kabla ya wakati wake, kila pumzi ilikuwa ni mapambano kwake kutokana na mapafu yake kutokomaa.

Tukio hili ni moja tu kati ya mengi mno yanayotokea nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka, takriban watoto 213,000 wanazaliwa njiti au wakiwa na uzito mdogo, na kati yao 13,000 hufariki dunia kutokana na matatizo yanayoendana na kuzaliwa kabla ya wakati.

Hii ni hali ambayo Vodacom Tanzania Foundation iliona inaweza kukabiliana nayo ipasavyo. Kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation, Vodacom Tanzania Foundation imekuwa ikitoa michango ya vifaa vya kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati kwenye vituo kadhaa vya afya katika mikoa ya Pwani, Tabora, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Lindi na Kigoma.

Mwaka jana misaada ya vifaatiba hivi ilitolewa katika kituo cha afya cha Muriet mkoani Arusha na ilikuwa na thamani ya Shilingi milioni 32, hospitali ya St. Mary’s Kibara iliyoko wilayani Bunda, mkoani Mara yenye thamani ya shilingi milioni 58 na kituo cha afya Inyonga kilichoko wilaya ya Mlele mkoani Katavi yenye thamani ya shilingi milioni 50.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mashine za oxijeni, mashine za kuleta joto kwa watoto, mirija ya kulisha, mablanketi, vipimo vya hewa ya Oksijeni na vifaa vingine muhimu kwa mahitaji ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Akizungumzia kazi ya asasi hiyo katika kunusuru maisha ya watoto njiti, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia alisema, “tunafarijika kusaidia kuboresha huduma za afya ya kinamama nchini kwa sababu ni eneo ambalo tunaona ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu. Kwa zaidi ya miaka kumi, asasi yetu imekuwa na msukumo wa kuboresha afya ya Watanzania kwa kutumia teknolojia ya mtandao wetu, kushughulikia mahitaji makuu ya kiafya ili kupunguza vifo vya akinamama nchini.”

Michango hii haijaishia tu katika mikoa iliyotajwa hapo juu bali imesambaa nchini kote na kutambulika kuwa na mafanikio makubwa. Hivi karibuni, asasi ya Vodacom Tanzania Foundation ilitambuliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kwa ushirikiano wake na Jumuia ya Msalaba Mwekundu nchini ambapo walichangia vifaa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma, ikiwa ni pamoja na vitanda vya watoto, mashine za kuleta joto na nyinginezo.

Mafanikio ya shughuli hizi yanapimika; kwa mfano wilayani Sengerema mkoani Mwanza, miradi ya Vodacom Tanzania Foundation imechangia kushusha vifo kwa asilimia 30 ya idadi ya vifo wilayani humo. Zaidi, shughuli hizi zinasaidia katika kujenga miundombinu ya afya ambapo baada ya kumalizika awamu ya kwanza, Moyo Center iliyoko katika hospitali ya CCBRT itakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wanawake 12,000 kwa wakati mmoja.

Tukirudi kwa Mama Hadija, kesi yake ina hatma nzuri pamoja na huzuni. Kumpoteza mtoto wake mchanga ni kidonda ambacho maumivu yake hadi leo yanasikika katika sauti yake akielezea mkasa wake. Anakumbuka vizuri sana siku zilizokuwa za wasiwasi na kukosa usingizi. Hata hivyo, anaendelea na maisha kutokana na kupona kwa mtoto wake wa pili.

Mtoto huyu, wa kike, alikuwa mtoto wa kwanza kufaidika na mchango wa vifaa vya mashine za joto, oksijeni na vingine vilivyotolewa na Vodacom Tanzania Foundation kwenye kituo hicho cha afya.

Akizungumzia aliyoyapitia anasema, “Ninaamini kuwa hata katika kipindi kigumu kabisa, Mwenyezi Mungu ana mpango wake. Nilivyofika kituoni hapa sikujua kuwa Vodacom walikuwa wametoa vifaa lakini mwanangu ndiyo akawa wa kwanza wilayani kwetu kunusurika kutokana na ukarimu huo wa Vodacom. Ninawaomba sana makampuni na watu wengine kutoa michango kama walivyofanya Vodacom kwani huwezi jua ni wakati gani unatumiwa kutimiza ndoto na sala za wengine.”



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2