WANAFUNZI WASIOFIKA SHULENI HUTOZWA FAINI YA SHILINGI ELFU TANO WILAYANI LUDEWA | Tarimo Blog


Na. Shukrani Kawogo, Njombe.

Wakazi wa kata ya Mavanga iliyopo wiliya ya Ludewa mkoani Njombe wamewalalamikia walimu wakuu pamoja na Afisa elimu wa kata hiyo kwa kuwalazimisha kulipia fedha kwa mtoto atakayeshindwa kufika shuleni pamoja na kuwalipa walimu wa kujitolea.

Wakitoa malalamiko hayo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga alipofanya ziara katika kijiji cha Mavanga, Mbugani pamoja na kitongoji cha Luhuhu getini wananchi hao wamedai kuwa walimu hao wamekuwa wakiwatoza kiasi cha shilingi elfu tano kwa siku na endapo mwanafunzi hatofika shuleni siku tano basi wanatakiwa kulipa elfu 25,000.

Melania Mtweve ni mmoja wa wananchi hao ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mavanga amesema wanashindwa kuelewa hizo fedha wanazitoa kwa malengo gani kwani wasipolipa watoto hurudishwa nyumbani mpaka aende na hiyo fedha.

" Kwa elimu ya mtindo huu ni bora watoto wangu wakaage nyumbani maana shule sasa hivi imekuwa ni mradi unaojitegemea ambao unawanufaisha walimu kwasababu mara nyingine mtoto anashinda shule kwa mambo ya msingi si kwa makusudi", Alisema Mtweve.

Sanjari na suala hilo pia wazazi hao wameiomba serikali kuajili walimu wa kutosha kwani wamekuwa wakilazimishwa kuchangia kiasi cha shilingi elfu 10,000 kwa kila mwanafunzi ili kuwalipa walimu wanaojitolea.

Akizungumza hayo mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Luhuhu getini David Mgaya amesema kuwa michango hiyo inawapa tabu sana kwani endapo mzazi anakuwa na watoto watano analazimika kulipa elfu 50, 000.

Mgaya ameiomba serikali kulichukulia suala hilo kwa uzito kwani wananchi wanahali ngumu na wanaposhindwa kulipa fedha hizo walimu wamekuwa wakiwasumbua watoto mashuleni ikiwemo kuwakamata wazazi na kuwapeleka katika ofisi za kijiji.

Akijibu hoja hizo afisa elimu wa kata hiyo Hosea Chaula amekiri kuwepo kwa malipo hayo ya kutofika shuleni na kuwalipa walimu wa kujitolea na kudai kuwa hayo yote yanatekelezwa kwa makubaliano kati ya kamati ya shule na wazazi.

Ameongeza kuwa wazazi na kamati hiyo ilikubaluana kuwalipisha fedha endapo watoto hawatafika shuleni ili kukomesha tabia za utoro kwa wanafunzia hao na kuwafanya wazazi wawe wanawahimiza watoto kufika shule.

Amesema kwa upande wa kuwalipa walimu wa kujitolea ni njia mojawapo ya kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora kutokana na uhaba wa walimu huku akitoa mfano wa shule ya msingi Ushindi ambayo ina wanafunzi 436 huku walimu walioajiliwa wakiwa sita hivyo wamelazimika kuongeza walimu wawili ambao hulipwa na wazazi hao.

"Haya yote tunatekeleza kwa mujibu wa makubaliano na wazazi na kwakuwa ni makubaliano nasi tunahakikisha tunafuatilia michango yote ambapo fedha ya walimu wa kujitolea hulipwa kwa awamu tatu kwa mwaka mwezi wa tatu, saba na tisa", Alisema Chaula.

Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amewataka viongozi hao wa elimu kufuata utaratibu wa utungaji sheria ndogo ndogo ambapo zinatakiwa kupitishwa na baraza la madiwani kwani ukusanyaji wa fedha kiholela ni sawa na kuiba.

Amesema kila malipo yaliyo halali yanapaswa kukatiwa risiti hivyo kama kunaulazima wa kutoza faini kwa mtoto asiyefika shule basi wapitishe sheria hiyo na wananchi wapewe risiti wafanyapo malipo hayo ikiwezekana ijulikane fedha hizo zinapikwenda.

Ameongeza kuwa suala la wazazi kuajili walimu hata bungeni amewahi kulizungumzia sambamba na kuiomba serikali kuleta walimu ambapo mpaka sasa tayari walimu 140 wameajiliwa wilayani Ludewa na bado anaendelea kupambana ili kupata walimu wengine zaidi.Hata hivyo amesema kuwa fedha hizo wanazotozwa wazazi kwaajili ya kuwalipa walimu wa kujitolea ni nyingi sana hivyo wanapaswa kupunguza kiwango cha malipo hayo.

"Nikweli serikali ina wajibu wa kuajili walimu lakini pia kwa nafasi yangu  nitaendelea kuishauri serikali iajili walimu hao wanaojitolea ili waweze kuwa wakudumu na kuingizwa katika mfumo na hiyo ya kutofika shule kuanzia leo naizika haitakuwepo tena kama watawadai waambieni waje wachukue kwangu na mnapokuja kwangu hakikisheni mnanipa na risiti", Alisema Kamonga.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia) akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mavanga.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) akipokea zawadi ya mkungu wa ndizi kutoka kwa mananchi mkazi wa kijiji cha Mavanga.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mavanga wakimlaki mbunge wao Joseph Kamonga baada ya kuwasili Kijiji hapo.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akiwagawia gazeti la mwananchi wakazi wa kijiji cha Mavanga ambalo ndani yake kuna makala iliyohusisha kijiji hicho.
Wananchi wa kitongoji cha Luhuhu getini wakiwa wamejiandaa na zawadi zao tayari kwa kumkabidhi mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia)
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia) akipiga ngoma huku wananchi wakiselebuka baada ya kuwasili kitongoji cha Luhuhu getini
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (aliyevaa suti) akiburudika pamoja na kikundi cha ngoma.

 Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto) wakijadiliana jambo na viongozi wenzake. Anayefuata ni Diwani wa kata ya Mavanga Daudi Luoga na katibu wa mbunge huyo Alphonce Mwapinga.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2