WATUMISHI WATATU WA SERIKALI AKIWEMO ASKARI POLISI, OFISA TRA WAKAMATWA KWA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA...WAKUTWA NA FEDHA ZA KIGENI | Tarimo Blog

Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV.


MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama wamefanikiwa kukamata kilo 99.33 za dawa za kulevya katika matukio tofauti zikihusisha watu nane kati yao watatu wakiwa ni watumishi wa Serikali.

Akizungumza leo Julai 19,2021 mkoani Dar es Salaam ,Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya amesema Juni 16, 2021 alizungumzia kuhusu kukamatwa kwa Kilo 88.27 za dawa za kulevya zikiwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado namba T503 DHC ikiwa imetelekezwa barabarani katika eneo la Kimara Korogwe mkoani Dar es Salaam.

"Niliwaambia kuwa tunaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.Kama nilivyo waahidi kuwa nitawataarifu juu ya matokeo ya uchunguzi; Katika uchunguzi uchunguzi wetu tulibaini kuwa, kati ya kilo 88.27 zilizokamatwa wakati ule kuna dawa nyingine ziliibiwa, na baadhi ya watumishi wasio waaminifu walishiriki kwenye uharifu
huo.

"Hivyo Juni 18, 2021 katika eneo la Mburahati Madoto NHC wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, tulifanikiwa kuwakamata mume na mke ambao ni Jamali Nangatukile( 45) na Mariyamu Bacha(28) wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 494.52.Juni 19 katika eneo la Bunju Beach tulimkamata aliyekuwa askari Polisi F.6763 CPL Deodatus Massare(37)akiwa na kilo 1.04 ya dawa za kulevya aina ya heroin.

"Aidha, Juni 21, 2021 katika maeneo ya Mivinjeni wilaya ya Temeke mkoani Dar es
Salaam, tulimkamata Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Andrew Paul(45) , mkazi wa Kurasini na wenzake Said Mgoha (45) maarufu kama Kindimu kazi yake fundi gereji mkazi wa mtoni kijichi, George Mwakang'ata (38) mfanyabiashara Mkazi wa Mtoni Kijichi, wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 1.02,"amesema Kusaya.

Ameongeza Juni 23 mwaka huu,walimkamata  Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Ally Juma Ally(32)  mkazi wa Kinyerezi mkoani Dar es Salaam pamoja na Abubakari Abdall(28) mfanyabiashara wakiwa na dawa za kulevya aina ya Methamphetamine yenye uzito wa gramu 597.61, Aidha, katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Ally  maeneo ya Zimbili Kinyererezi, walimkuta akiwa na fedha Sh.82,043,000 na Dola za Marekani  5100.

"Watuhumiwa wote wameshafikishwa mahakamani wakikabiliwa na makosa ya  kujihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za Kulevya makosa ambayo ni Uhujumu  Uchumi kwa Sheria za Nchi yetu. Pamoja na hatua hii tuliyofikia bado tunaendelea na  uchunguzi ili kuwabaini waharifu wengine walioshiriki katika tukio hilo.

"Natoa onyo wa wale wanaotaka kujaribu makali ya Serikali kwa kuendeleza au kujihusisha na biashara hii haramu, ninawaonya waachane na biashara hii na badala  yake wajikite katika biashara na shughuli nyingine halali za kujiongezea kipato. Mamlaka tuko macho usiku na mchana, tutawakamata katika siku wasiyoijuana watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,"amesema.

Pia amewaaomba  waandishi kuendelea kutumia kalamu zao kuwapa elimu watanzania na jamii kwa ujumla kuhusu madhara yatokanayo na biashara na matumizi ya dawa za kulevya, kwani janga hilo lisiposhughulikiwa katika umoja nguvu kazi ya taifa letu itapotea.

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2