Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ufaransa nchini wamefanikisha mafunzo ya kozi fupi ya lugha ya Kifaransa kwa baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo kama sehemu ya kuwajengea uelewa wa kufahamu lugha zaidi ya moja.
Akizungumza leo wakati wa tukio la kukabidhi vyeti kwa watumishi hao waliojifunza lugha hiyo kwenye Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa jijini Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Anisa Mbaga amesema uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili ndio uliosababisha watumishi hao kupata fursa ya kujifunza lugha hiyo.
"Serikali ya Tanzania na watanzania pamoja na Serikali ya Ufaransa na watu wa Ufaransa wamekuwa na uhusiano mzuri, lakini pia juhudi za Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula pamoja na viongozi wengine wa Wizara hiyo ambao waliomba Ubalozi wa Ufaransa kutoa mafunzo mafupi ya lugha hiyo kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
"Kama tunavyofahamu Wizara yetu inahusika na mashirikiano kati yetu na nchi nyingine , kwa hiyo kupata uelewa wa lugha zaidi ya moja kwa watumishi wa Wizara yetu ni nyenzo na muhimu katika kutekeleza majukumu ya kila siku.Ni muhimu sana kwa watumishi wetu kufahamu lugha zaidi ya moja , tunao watumishi ambao wanafahamu Kifaransa lakini wapo hatua ya chini.
"Hivyo Wizara inaendelea na jitihada za kuendelea kuwajengea uwezo watumishi ili kuwawezesha kufahamu lugha zaidi ya mmoja.Wengi wanafahamu Kingereza , hivyo kuongeza na Kifaransa ni hatua nzuri na muhimu kwani kuna nchi ambazo tunashirikiana nazo na zinazungumza Kifaransa,"amesema Balozi Mbaga ambaye kwenye tukio hilo alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Joseph Sokoine.
Ameongeza kuhitimu kwa watumishi hao katika hatua ya kwanza na wengine hatua ya kati ya lugha ya Kifaransa sasa itasaidia sana kuwawezesha katika kutekeleza majukumu yao na watakapokutana na wana diplomasia wengine wanaotumia lugha hiyo itakuwa rahisi kuwasiliana na kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier ametoa pongezi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula kwa kuona muhimu wa watumishi wa Wizara hiyo kupata mafunzo mafupi ya lugha ya Kifaransa kama sehemu ya kuwawezesha watumishi hao kuelewa lugha hiyo ili kurahisisha mawasiliano kati yao na nchi nyingine zinazoongea lugha ya Kifaransa.
Amesema lugha ya Kifaransa ni kati ya lugha ambazo zinazungumwa na mamilioni ya watu duniani kote, hivyo kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni hatua nzuri na kwamba Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo hiyo ya kuhakikisha lugha za nchi hizo mbili zinafundishwa na kuenezwa kwa pande zote.
"Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ambao wamepata fursa hii wapo ambao wamejifunza hatua ya mwanzo kabisa na wengine wamejifunza hatua ya kati , hivyo bado wanayo nafasi ya kujiendeleza ili kuifahamu vema lugha ya Kifaransa,"amesema Balozi Clavier na kuongeza kuwa idadi ya wanaotumia lugha ya Kifaransa duniani imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.
Mmoja ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Amos Tengu anayetokea kitengo cha Diaspora amesema wamekuwa kwenye mafunzo kwa wiki tatu, hivyo wanaishukuru Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ufaransa kufanikisha mafunzo hayo ya Kifaransa.
"Kama mnavyofahamu Wizara ya Mambo ya Nje kutokana na kusimamia masuala yake mbalimbali kwa kushirikiana na nchi za nje maana yake kuna kunakuwa na muingiliano na lugha ya Kifaransa ni lugha ya kimataifa na kwa Afrika katika nchi 56 , nchi 26 zinaongea kifaransa. Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania amezungumzia ukubwa wa lugha hii na idadi ya watu wanaoizungumza,"amesema Tengu.
Ameongeza kwa wao kufahamu lugha hiyo inasaidia kwenye mawasiliano na kwamba wanatumia lugha ya Kingereza lakini kuna nchi nyingine ambazo zinatumia Kifaransa , hivyo kufahamu lugha hiyo ni muhimu na bahati nzuri wengi ambao wamejifunza hasa wale wa hatua ya mwanzo wameahidi kuendelea na wale ambao wamejifunza hatua ya kati nao wanataka kuendelea zaidi.
"Kifaransa nacho kina hatua zake, kuna hatua ya kuanzia awali hadi hatua ya juu kabisa, kwa sisi wengine angalau tunakijua Kifaransa lakini tunatamani kufahamu kwa hatua kubwa zaidi.Hivyo niseme tunashukuru Wizara yetu kwa kutambua umuhimu wa kutuwezesha kupata mafunzo haya ingawa kwa maoni yetu ambao tumepata mafunzo tunasema wiki tatu hazitoshi, tunahitaji muda mrefu zaidi ili kuifahamu vema lugha hii,"amesema Tengu.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment