Naibu Waziri Mawanaidi atoa maagizo kwa uongozi wa Wilaya kupata taarifa ya mwenendo wa kesi hizo.
Na Mwandishi Wetu, Kibondo Kigoma
Vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto vimebainika kukita mizizi katika wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma ambapo ripoti ya Wilaya hiyo inaonesha kuwa watoto 981 wamepewa ujauzito katika kipindi cha miezi sita iliyopita Januari mpaka Juni 2021.
Taarifa hiyo imebainika wakati Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa wilayani humo kukagua na kujionea utoaji wa huduma za ustawi wa Jamii na masuala ya maendeleo ya jamii.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema taarifa hizo haziwezi kufumbiwa macho na badala yake watendaji wanaohusika wafanye kila linalowezekana kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na haki inatendeka katika kipindi kifupi iwezekanavyo.
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi ameongeza kuwa jamii haiwezi kutegemea miujiza ya mafanikio ya kizazi kijacho endapo itabaki kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani dhidi ya wanawake na watoto kwa kuangalia watoto wao wanapata mimba katika umri mdogo na kukatisha ndoto zao.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi amezindua Kituo cha huduma jumuishi kwa wahanga na waathirika wa vitendo vya ukatili wa Kijinsia (One Stop Centre) katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma kitakachowawezesha walengwa wake kupata huduma kwa pamoja na kwa muda mfupi na kuwataka maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii kushirikiana na vyombo vya dola kutoa elimu kwa kina dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Amesema kuwa kupitia Kituo hicho ambacho kimefadhiliwa na Shirika la kimataifa la Save the Children, kinajumuisha ofisi za polisi, maafisa ustawi, Daktari kitawezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa pamoja kwa waathirika ndani ya muda mfupi.
Kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto Naibu Waziri amesema kuwa Sheria ya Mtoto inataja mashauri yao kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita lakini kwa mazingira ya huduma za mkono kwa mkono kuna umuhimu wa kumaliza shauri ndani ya muda mfupi zaidi.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo Sophia Gwamagobe amepongeza juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kutafuta mwarobaini wa matatizo miongoni mwa Watanzania ikiwemo kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Save the Children Jackson Nsabo amesema Shirika hilo limewiwa kujenga kituo cha mkono kwa mkono ili kukabiliana na wimbi la vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Awali, Naibu Waziri Mwanaidi alitembelea kikundi cha malezi chanya Wilayani Kibondo ambacho mbali na kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa vitendo vya ukatili, kinajishughulisha na ujasiriamali kwa kutengneza sabuni.
Akiwa kituoni hapo, amewataka wazazi na walezi nchini kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao ili kujenga taifa lenye ustawi kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amehitimisha ziara ya kikazi ya siku tano Mkoani Kigoma kwa kutembelea shughuli za Maendeleo na Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Wilaya Kigoma vijijini, Buhigwe, Kasulu na Kibondo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment