BALOZI wa Tanzania Nchini China, Mbelwa Kairuki amewatoa hofu Watanzania wanaofanya biashara zao nchini humo kuwa hali ni nzuri na kwamba serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea na majukumu yake ya ujenzi wa Taifa.
Balozi Kairuki ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara hao ambapo amesema mkazo wa Serikali hivi sasa ni katika kuhami uchumi wa Nchi ambao unakabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa Uviko-19.
Amesema mbali ya kuhami uchumi Serikali pia inaendelea kushughulika vema na janga lenyewe la Corona ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kupata chanjo ambayo itatolewa kwa wananchi wake bure kabisa ikiwa ni jitihada za kupambana na ugonjwa huo.
" Niipongeze Serikali yetu chini ya Rais Samia kwa kuhamasisha inapeleka chanjo kwa wananchi wake na chanjo hiyo inatolewa kwa hiyari, lakini pia nitoe rai kwenu nyinyi ndugu zetu hapa kwa uzoefu wenu mlioupata hapa China muendelee kutoa hamasa na elimu kwa ndugu waliopo Tanzania katika kuchukua tafadhari za ugonjwa.
Lakini siyo tu kuwahamasisha kuvaa Barakoa na kuepuka misongamano pia mtoe elimu kwao na hamasa katika jambo hili la kuchoma chanjo Ili kuwaondoa hofu Watanzania wenzetu waliopo nyumbani," Amesema Balozi Kairuki.
Amesema eneo lingine ambalo limeathiriwa na Corona ni kwenye eneo la usafirishaji wa mizigo kutokana na Kampuni nyingi za Meli kupunguza Safari za kwenda Tanzania na sehemu nyingine Duniani hivyo tumechukua hatua za kuzungumza na makampuni ambapo wamesema ugonjwa ndio Sababu ya wao kusimamisha safari zao.
" Niwahakikishie kuwa tunaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii ya usafiri wa majini lakini nafurahi kuwaambia kuwa Shirika letu la Ndege la Air Tanzania ambapo limeanza safari zake kutoka Gouzoung China kwenda Dar es Salaam China na kibali walichopewa ATCL ni Cha kusafirisha mizigo kwa wiki mara moja.
Kwa sasa kwa vile bado wafanyabiashara wengi hawajaisikia fursa hii ATCL itaanza safari zake mara moja kwa wiki mbili na baadaye wateja wakiongezeka ndivyo pia tutakavyoongeza safari zetu," Amesema Balozi Kairuki.
Amesema safari hizo zitakua zinatoka China kwenda Dar es Salaam, Zanzibar na miji mingine ambapo Ndege hizo zinaenda ikiwemo Entebbe Uganda, Lusaka Zambia, Harare Zimbabwe n Comoro.
"Nitoe wito kwenu kuchangamkia fursa hii ambayo Serikali yetu imetoa ya Ndege hii ya mizigo na itakua inaondoka Dar es Salaam siku ya Ijumaa saa tano asubuhi na kuwasili Jumamosi China saa tisa alfajiri, na itaondoka tena China Jumamosi hiyo hiyo saa 11 alfajiri na kufika Dar es Salaam Jumamosi saa tano," Amesema Balozi Kairuki.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment