Benki ya NBC yaendelea kuwagusa wakulima kupitia bima ya Afya | Tarimo Blog

 Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano rasmi  na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) yanayolenga kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kuingia kwenye mfumo wa huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya.

Mpango huo utatekelezwa na  benki ya NBC  kwa kuwasilisha michango ya  Bima ya afya moja kwa moja  katika Mfuko  wa Taifa wa Bima ya afya  kwa niaba ya wakulima watakaokuwa na Akaunti Benki ya NBC na kuchukua mikopo ya kilimo kupitia benki hiyo.

Wakizungumza kwenye hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw Bernard Konga walisema mpango huo unalenga kuongeza wigo  wa wananchi hususani wakulima katika mfumo wa Bima ya afya na hivyo kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya kujenga uchumi imara wakiwa na afya njema.

“Sisi kama benki ili tuweze kuendelea kufanya vizuri zaidi tunahitaji kuwa na uchumi imara ambao kimsimgi pia unategemea nguvu kazi yenye afya njema. Suala la huduma  afya ya uhakika kwa wateja wetu wakiwemo wakulima na moja ya vipaumbele vyetu na ndio sababu hatukusita kuunga mkono mpango huu wa Ushirika Afya,’’ alisema Bw Sabi.

Kwa mujibu wa Bw Sabi, kupitia mpango huo mkulima atachangiwa  kiasi cha sh 76,800 kwa mwaka na ikiwa  mkulima ana mwenza wake  nae atachangiwa kiasi cha sh 76800 ambapo pia kila mtoto atachangiwa sh 50,400 kwa mwaka.

“Bima hii itatolewa na NHIF na itapatikana kwenye matawi yote ya NBC nchi nzima hivyo naomba wakulima wachangamkie fursa hii. Kwa upande wetu maofisa wa benki wamejipanga kuwatembelea wakulima wanachama wa ushirika kuhakikisha wanawapatia habari hii njema kupitia benki ya NBC,’’ aliongeza Bw Sabi.

Kwa upande wake Bw Konga aliwahakikishia wakulima wote watakaojiunga na mpango huo kwamba  watapata huduma bora kwa urahisi  zaidi huku akibainisha kuwa taasisi hiyo imejipanga kurahisisha huduma  kupitia maboresho  ya mfumo wake wa TEHAMA.

“Nina imani kupitia ushirikiano wa kihuduma baina ya NBC na wakulima kote nchini mpango huu utakuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa lengo haswa ni kuwafikia wakulima popote walipo ili tuweze kuongeza wigo wa wanufaikaji wa mfuko huu,’’ alisema Bw Konga ambae alibainisha kuwa hadi kufikia sasa ni asilimia 8 tu ya watanzania ndio wanatumia huduma hiyo ya bima ya afya kupitia mfuko huo.

Kwa upande wake Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Tanzania Dk. Benson Ndiege pamoja na kuzipongeza taasisi hizo mbili kwa makubaliano hayo muhimu alisema ili mpango huo ufanikiwe vizuri ipo haja ya kuhakikisha vyama vya ushirika nchini vinajiimarisha zaidi ili wakulima waendelee kuwa katika mfumo rasmi ambao ndio nguzo ya  mpango huo.

“Zaidi pia napenda kusisitiza kwamba kupitia mpango huu wakulima wahakikishiwe wanapata huduma bora kama ilivyokusudiwa ili kuwavutia wakulima wengine wengi zaidi. Hata hivyo sina hofu na ufanisi wa mpango huu kwa kuwa nafahamu vema uimara wa taasisi hizi mbili yaani NBC na NHIF,’’ alisisitiza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi  (Kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw Bernard Konga (Kulia) wakionesha hati za makubaliano baina ya taasisi hizo mbili yanayolenga kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kuingia kwenye mfumo wa huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya. Anaeshuhudia ni Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Tanzania Dk. Benson Ndiege (Katikati)


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi  (Kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw Bernard Konga (Kulia) wakisaini hati za makubaliano baina ya taasisi hizo mbili yanayolenga kuwawezesha wakulima walioko ndani ya vyama vya ushirika nchini kuingia kwenye mfumo wa huduma za matibabu kupitia mpango wa bima ya afya kwa wakulima unaojulikana kama Ushirika Afya. Anaeshuhudia ni Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Tanzania Dk. Benson Ndiege (Katikati)


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi  (Kushoto) akimkabidhi zawadi kutoka benki hiyo  Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw Bernard Konga (Kulia) wakati wa hafla hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi  (Kushoto) akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi  (Kushoto) akimkabidhi zawadi kutoka benki hiyo  Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw Bernard Konga (Kulia) wakati wa hafla hiyo.





Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2