BILIONI 65 KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI GOBA, MAKONGO | Tarimo Blog

 

Na Mwandishi wetu, Michuzi TV
MKUU Wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla leo Agosti 27 ametembelea miradi mitatu mikubwa ya maji ikiwemo kituo cha kusuma maji cha Makongo juu, ujenzi wa tenki la maji la Tegeta A lenye ujazo wa lita milioni 5 na ujenzi wa tenki la maji Bunju lenye ujazo wa lita milioni 5 miradi inayosimamiwa na Mamlaka Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA.) Huku ikitegemewa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Akiwa katika mradi mkubwa wa maji wa Tegeta A unaogharimu shilingi bilioni  65 Makalla amesema mradi huo utawanufaisha wakazi wengi wa maeneo hayo na kuipongeza DAWASA kwa kusimamia vyema miradi ya maji katika Mkoa huo.

Amesema kuwa ziara yake kwenye mradi hiyo ni kuangalia namna bora ya kuthibiti changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo yaliyopo pembezoni wa mji ikiwemo Mabwepande, Mbweni, Bunju, Wazo, Salasala, Goba, Kinzudi, Changanyikeni na Mivumoni kwa kuhakikisha wananchi  wanapata huduma ya maji na kueleza kuwa amejiridhisha na namna mradi huo unavyoendelea hasa kwa mantenki yanayojengwa.

Makalla amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 mkoa wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla upatikanaji wa maji uwe kwa asilimia kubwa.

Aidha ametaka DAWASA kuendeleza juhudi hizo kwa kasi zaidi na kuyafikia maeneo mengi zaidi hasa yale ambayo yamepitiwa na bomba kubwa la maji lakini wanakosa huduma hiyo.

''Niwatoe hofu wananchi kwa miradi hii  wakazi wa Dar es Salaam changamoto ya maji inakwenda kuwa historia, Serikali ipo nanyi na inaposema kuwa upatikanaji wa maji Mkoa wa Dar es Salaam ni aslimia 92  basi wote tusimame hapo.'' Amesema.

Pia ameipongeza DAWASA kwa usimamizi bora wa miradi ya maji na kuwataka kuendelea na kasi hiyo katika kuhakikisha kila mwananchi mkoani hapo  anafikiwa na huduma  ya maji safi na salama.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ubora na Viwango kutoka DAWASA Injinia Christopher Christian aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja  amesema, mradi wa maji wa Tegeta A ni mradi mkubwa unaoanzia Bagamoyo hadi Chuo cha Ardhi na ni uendelezaji wa uwekezaji wa Serikali na unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya dunia na kusimamiwa na mkandarasi kutoka China na Benki ya dunia kwa gharama ya shilingi Bilioni 65 za kitanzana bila kodi.

Amesema, katika awamu ya kwanza maeneo mbalimbali ikiwemo Tegeta A yalipitiwa na mradi wa ujenzi wa vituo vya awali (visima vya maji) vya kusukuma na kupokea maji lakini upatikanaji wa maji ukawa hafifu kutokana na miinuko kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Tegeta A.

Injinia Christopher ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya kwa ushirikiano wanaoutoa na kusisitiza kuwa  maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa yatatekelezwa na wakazi wa maeneo yaliyokuwa yanapata maji kwa kiasi yatapata maji zaidi na yaliyokosa maji yatapata maji safi na salama kwa uhakika mwishoni mwa mwaka huu.
Mkuu wa kitengo cha ubora na viwango kutoka DAWASA Injinia Christopher Christian akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kuhusu mradi wa kituo cha kusukuma maji  kilichopo katika Kata la Makongo Juu katika Manispaa ya Kinondoni mkoani wa Dar es Salaam  unavyotoa huduma wakati wa ziara yake ya kutembelea Miradi ya DAWASA inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe 
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla akionesha maeneo ambayo bado yana changamoto ya upatikanaji wa maji mara baada ya kupata maelezo ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Makongo Juu wakati wa ziara ya kutembelea Miradi inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe.
Mkuu wa kitengo cha ubora na viwango kutoka DAWASA Injinia Christopher Christian (wa pili kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kuhusu kituo cha kusukuma maji pamoja na usambazaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam uliopo katika Kata la Makongo Juu katika Manispaa ya Kinondoni mkoani humo  wa kati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ritamaty Lwabulinda.
Muonekano wa  mitambo za kusukumia maji iliyopo kwenye mradi wa Makongo Juu katika Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar Es Salaam.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla akizikiliza maelezo yaliyokuwa yanatolewa  na Msimamizi wa Mradi wa DAWASA, Mhandisi Ishmael Kakwezi(wa kwanza kushoto) kuhusu ujenzi wa tenki la Tegeta A ujenzi wa tenki la maji la Tegeta A ambalo litakalokuwa na ujazo wa Lita milioni tano wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na DAWASA.
Ujenzi wa tenki la maji la Tegeta A ukiendelea
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe wakiendelea na ziara ya ukaguzi wa mradi wa tanki la Tegeta A mbalo litakalokuwa na ujazo wa Lita milioni tano. Pamoja na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ritamaty Lwabulinda
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupata maelezo na kukagua ujenzi wa Tanki la Tegeta A litakalokuwa na ujazo wa Lita milioni tano wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na DAWASA.
Mkuu wa kitengo cha ubora na viwango kutoka DAWASA Injinia Christopher Christian akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ya kupata maelezo na kukagua ujenzi wa Tanki la Tegeta A wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji.
Mkuu wa kitengo cha ubora na viwango kutoka DAWASA Injinia Christopher Christian akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla namna watakavyoweza kulaza kulaza mambomba kwa ajili ya kusambaza maji katika eneo la Madale na maeneo mbalimbali ya manispaa ya Kinondoni.
Baadhi ya Mabomba yaliyopo eneo la Madale yatakayotumika kusambazia maji 
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadi ya viongozi wa DAWASA na mkandawasi wakati wa Ziara ya Mkuu wa Mkoa alipokuwa anakagua miradi wa maji inayotekelezwa na DAWASA. Katikati ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ritamaty Lwabulinda
Ujenzi wa tenki la maji la Bunju ukiendelea
Mkuu wa kitengo cha ubora na viwango kutoka DAWASA Injinia Christopher Christian(wa tatu kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla(wa pili kulia) kuhusu ujenzi wa tenki la maji la Bunju litakalokuwa na ujazo wa Lita milioni tano wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na DAWASA. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla akitoa majumuhisho kwa waandishi wa habari kuhusu ziara yake aliyoifanya ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) mara baada ya kukagua ujenzi wa tenki la maji la Bunju litakalokuwa na ujazo wa Lita milioni tano.

 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2