Na Rahma Taratibu,WFM-DSM
SERIKALI imesema kuwa uzoefu kutoka Nchi mbalimbali unaonesha kuwa matokeo chanya katika ukusanyaji wa mapato yanaweza kupatikana kwa kufanya mapitio na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji mapato na hivyo kushauri kuwa ni muhimu kwa sasa Tanzania nayo ikafanya hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba katika uzinduzi wa Tume ya Kutathimini na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na matumizi ya Serikali.
Dk Nchemba amesema tathmini ya kina itasaidia kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia suluhisho ili kuboresha hali iliyopo ya makusanyo ya mapato ya Serikali.
Amesema kuwa ni imani yake kuwa Tume hiyo aliyoizindua leo itakuja na mapendekezo yatakayoboresha mfumo uliopo pamoja na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali na hivyo kuwa na bajeti endelevu.
Ametaja majukumu ya Tume hiyo kuwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mfumo wa kibajeti na kupendekeza namna bora ya kuiwezesha Serikali kuwa na bajeti endelevu, Kufanya ulinganishi wa Mfumo wa Kodi wa Tanzania na nchi nyingine zinazofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
" Kupitia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mifuko yenye vyanzo maalum na kushauri ipasavyo iwapo kuna haja ya kuendelea nayo au vinginevyo kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa bajeti ya Serikali;
Kufanya tathmini ya mwenendo wa nakisi ya bajeti ya Serikali na kutoa mapendekezo kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya Serikali;
Kufanya tathmini ya ukuaji na ugharamiaji wa deni la Serikali, ulipaji wa mishahara, ulipaji wa malimbikizo ya madai/madeni na ukuaji wake na kupitia gharama na taratibu za uanzishaji na uendeshaji wa biashara hapa nchini na kupendekeza namna ya kuboresha kodi zinazotozwa ili kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji wa biashara hapa nchini," Amesema Dk Nchemba.
Amesema kazi kama hii iliwahi kufanyika mwaka 1991 ambapo Tume iliyoundwa kipindi hicho ilikuja na mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kufutwa kwa kodi na tozo mbalimbali zilizoonekana kuwa kero pamoja na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo yameleta matunda makubwa katika ukusanyaji wa mapato.
Dk Nchemba amesema anatambia kuwa Tume hiyo imejumuisha wajumbe wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya uchumi, kodi, fedha na mifumo ya matumizi ya serikali ambapo wajumbe hao wametoka kwenye Taasisi zilizopo pande mbili za Muungano.
Amesema katika hali ya kawaida kiwango cha ukuaji wa uchumi kinatarajiwa kuendana na ukuaji wa mapato ya ndani yanayoweza kutosheleza ugharamiaji wa matumizi ya serikali ambayo nayo yamekua yakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Tume hiyo yenye wajumbe 10 inayoongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Samweli Wangwe, itafanya kazi hiyo kwa muda wa miezi 6 kuanzia tarehe 25 Agosti, 2021 .
Waziri wa Fedha na Mpiango Mh. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati akizindua Tume ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali uliofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania BoT jijini Dar es salaam leo.
Mjumbe wa Tume ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali,Profesa Nehemiah Osorro akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania BoT jijini Dar es salaam leo.
Baadhi ya wajumbe wa Tume ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya Serikali wakiwa katika uzinduzi huo.
Picha ya wajumbe wa Tume wakiwa pamoja.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment