DKT. SENGATI ATAKA WAKUU WA WILAYA KUHAKIKISHA UHAKIKA WA CHAKULA SHULENI | Tarimo Blog


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akisaidia ujenzi wa jengo la kufulia nguo la Hospitali ya Halmashauri ya Msalala kwa kupokezana ndoo ya udongo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Bw.Mabala Mlolwa wakati wa ziara ya kamati ya Siasa ya kujionea ujenzi wa hospitali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akitoka ndani ya jengo la wagonjwa wa nje la Hospitali ya Halmashauri ya Msalala pamoja na mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ambaye jina lake halikujulikana mara moja wakati wa ziara ya kamati ya Siasa ya kujionea ujenzi wa hospitali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati wakiwa katika jengo la Mahabara ya moja ya Shule ya Sekondari ambayo yeye na kamati ya Siasa ya Mkoa pichani walifika na kufanya ukaguzi wa ujenzi wa Mahabara hiyo katika Halmashauri ya Msalala Shinyanga.


Na Anthony Ishengoma-Shinyanga

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ameiambia kamati ya Siasa ya Mkoa wa Shinyanga kuwa suala la chakula shuleni ni agenda muhimu katika mkoa wake kwasababu mwanafunzi anapopata chakula shuleni inamsaidia kufuatilia zaidi masomo yake.

Dkt. Sengati ametoa rai hiyo wakati wa ziara ya siku moja ya kamati ya siasa ya mkoa ilipotembelea Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama kujionea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri hiyo kama hatua muhimu ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi.

Dkt. Sengati  amesisistiza kuwa ili dhamira yake ya kuhakikisha kuna chakula shuleni itimie atatoa agizo kwa maandishi ili Wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri waweze kuhakikisha wanafunzi wa sekondari wanapata chakula na wale wa shule za masingi wanapata uji kwa shule zote za mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Sengati ameongeza mkoa wa Shinyanga pamoja na masuala mengine muhimu anataka uwe na matokeo mazuri katika mitihani ya Taifa ili uweze kuwa katika mikoa kumi bora nchini na ili kufikia hatua hiyo ni lazima kuwe na mazingira mazuri ya kujifunza lakini pia yale ya kujifunzia.

Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Shinyanga pia likagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Msalala ambapo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Bw. Mabala Mlolwa amaeutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo ifika Agosti 30 mwaka huu.

Bw. Mabala ameongeza kuwa inawezekana kukawa na kasoro ndogo ndogo lakini hospitali hiyo lazima ianze kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa kuanza kwa hospitali hiyo itakuwa ni hatua kubwa ya kutatua changamoto zilizopo lakini pia kero mbalimbali zinazoikabili jamii hiyo.

Kamati hiyo siasa pia likagua maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala na kujionea maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo na kuonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mkandarasi wa jengo hilo SUMA JKT ambaye kimsingi ni wakala wa Serikali chini ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Aidha Muhandisi wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Fransisko Magoti aliiambia kamati hiyo kuwa kwa mkataba uliopo kati ya Halmashauri na mkandarasi huyo ni kwamba ifikapo Desemba mwaka huu kama hatakuwa hajakamilisha upande mmoja wa jengo hilo ili uanze kufanya kazi mkataba huo utabadilika na atafanya kazi kama kibarua kama ilivyo kwa akaunti ya dharula.

‘’Kama atashindwa kukamilisha ilivyo katika mkataba mkandarasi huyu atakuwa akifanya kazi kwa mtindo wa akaunti ya dharula kwa hiyo tutakuwa tunamuita kila wakati ambao tutakuwa na fedha kwa kuwa mfumo wa sasa wa kandarasi unatekelezeka kwa fedha ambayo tayari tunayo kulingana na ukubwa wa jengo hili’’.Alifafanua Muhandisi Magoti.

Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Shinyanga iliendelea na ziara yake katika Manispaa ya Kahama na kujionea miradi mitatu katika Manispaa hiyo na inaendelea na ziara yake kujionea miradi kama hiyo kwa Halmashauri nyingine nne zinazounda Mkoa wa Shinyanga.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2