Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Simon Sirro akimkabidhi Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala tuzo ya heshima kwa kudhamini zoezi zima la kufanya mapitio ya Mwongozo wa Jumla wa Utendaji Kazi wa Jeshi la Polisi (Police General Orders) uliokamilika na kuzinduliwa rasmi leo jijini Dar es Saalam. Anyeshuhudia pembeni kulia ni Meneja wa Mawasiliano LSF, Jane Matinde.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala akizungumza leo Jijini Da r es Salaam na Maafisa Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi pamoja na Makamanda wa Mikoa na Vikosi wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Jumla wa Utendaji Kazi wa Jeshi la Polisi (Police General Orders), ambao utawezesha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi nchini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Simon Sirro leo Jijini Dar es Salaam wakizindua Mwongozo wa Jumla wa Utendaji Kazi wa Jeshi la Polisi (Police General Orders) baada ya kuufanyiwa marekebisho mbalimbali yatakayowezesha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi pamoja na kurasimisha madawati ya kijinsia na watoto ndani ya jeshi hilo kama sehemu ya mkakati mzuri wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Wa kwanza kulia anayeshuhudia ni Kamishna wa Utawala na Menejiment ya Rasilimali watu, Benedict Wakulyamba.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala akiwa na tuzo ya heshima mara baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Simon Sirro kwa kutambua mchango wa LSF katika kusaidia zoezi la marekebisho Mwongozo wa Jumla wa Utendaji Kazi wa Jeshi la Polisi (Police General Orders) mbalimbali yatakayowezesha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi nchini.
JESHI la Polisi nchini Tanzania leo Agosti 25, 2021 limezindua mwongozo wa jumla wa utendaji kazi wa jeshi la polisi (Police General Order) baada ya kuufanyia marekebisho mapya, ambayo yanalenga kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa jeshi hilo nchini.
Marekebisho ya mwongozo huo yanalenga kulifanya jeshi la polisi kuendelea kufanya shughuli zake kwa weledi na kuongeza uwajibikaji zaidi wa jeshi hilo katika kushughulikia masuala mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Pamoja na mambo mengine maboresho ya mwongozo huo mpya unajumuisha urasimishaji wa madawati ya kijinsia na watoto ndani ya jeshi hilo kama sehemu ya mkakati mzuri wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Uzinduzi wa mwongozo huo umekuja kufuatia Jeshi la Polisi kuona haja ya kutafuta wadau watakaosaidia kufanikisha mchakato huo mkubwa unaolenga kuleta ufanisi na ubora wa huduma ya jeshi hilo katika kutimiza wajibu wake wa kulinda usalama wa raia wote nchini.
Kutokana na uhitaji wa maboresho ya mwongozo huo, Jeshi la Polisi nchini liliingia makubaliano na Shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania, Legal Services Facility (LSF), ambapo LSF lilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendesha mchakato mzima wa kupitia upya mwongozo uliokuwepo awali na kuangalia maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa zaidi ili kuendelea kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini.
Ikumbukwe kuwa, kwa muda mrefu Jeshi la Polisi limekuwa likilinda na kutetea haki na usalama wa raia na mali zao, ambapo kupitia madawati ya kijinsia na watoto yamekuwa yakitumika zaidi ndani ya chombo hicho kutatua kesi mbalimbali zinazohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto kama kundi maalum katika jamii.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro, amesema anayo furaha sana kushirikiana na shirika la LSF katika kufanikisha zoezi zima la kupitia na kurekebisha mwongozo wa Jeshi la Polisi nchini, ambao sasa utasaidia kuwalinda zaidi wanawake na watoto kama kundi maalum linalohitaji uangalizi kutokana na ukweli kuwa, kundi hilo ndio limekuwa likiathirika zaidi na vitendo vya ukatili nchini.
“Kwakweli sisi kama Jeshi la Polisi nchini tumekuwa tukifanya kazi kubwa chini ya mwongozo wetu kuhakikisha kuwa, tunalinda usalama wa rai ana mali zao.
Lakini kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini ilitulazimu kuanzisha madawati maalumu ya jinsia na watoto ndani ya jeshi letu ili kushughulikia tatizo hili;
“Uundwaji wa madawati haya ilikuwa ni jitihada mahususi za kiu ya kutaka kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya ukatili mbalimbali ingawaje madawati haya hayakuwa yameingizwa rasmi katika Amri ya Jumla ya Jeshi la Polisi au Mwongozo wa Jumla wa Utendaji wa Jeshi la Polisi,” amesema IGP Sirro
IGP Simon Sirro ameongeza kuwa mwongozo uliozinduliwa leo licha ya kutambua rasmi uwepo wa madawati ya jinsia, mwongozo huo utatambua rasmi pia Mtandao wa Askari Wanawake kama sehemu muhimu ya jeshi hilo kuendelea kukabiliana na kesi za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto nchini.
“Ndani ya Jeshi la Polisi kuna Mtandao wa Askari Wanawake nchi nzima ambao nao umekuwa ukifanya kazi nzuri kila kukicha kuhakikisha haki na ustawi wa maendelo ya wanawake na watoto unalindwa.
Katika maboresho yaliyofanyika ya mwongozo wetu mtandao huo nao umerasmishwa pia ili kuchochea jitihada zetu pamoja kama jeshi kuendelea kulinda usalama wa raia wote hususani wanawake na watoto,” ameongeza IGP Sirro.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa kukamilika kwa mapitio na maboresho ya mwongozo wa Jeshi hilo ili kusimika ama kutambua rasmi jitihada zilizokuwepo kama vile madawati ya jinsia na mtandao wa askari wanawake ndani ya jeshi hilo ni sehemu ya mkakati maalumu wa LSF kushirikiana na serikali pamoja na taasisi zake katika kufanya uchechemuzi, ili kuleta mabadiliko ya kisera, sheria na miongozo mbalimbali nchini, itakayoboresha zaidi ustawi wa haki na maendeleo ya wanawake na wasichana nchini.
“Uzinduzi huu una maana kubwa sana kwetu kama shirika binafsi linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania. Hii ni sehemu ya ushirikiano wetu na Jeshi la Polisi kupitia makubaliano tuliyotiliana saini ili kuweza kusaidia zoezi la kuupitia upya mwongozo wao ili kurasmisha kabisa madawati ya jinsia, ambayo yamekuwa yakifanya kazi kubwa ya kulinda na kutetea haki za wanawake na watoto nchini Tanzania.
Vilevile Ng’wanakilala ameeleza kuwa mwongozo wa utendaji wa polisi ambao umeboreshwa anaamini kuwa utakwenda kusaidia watu wote hasa wanawake na watoto, ambao wamekuwa ndio kundi linalohitaji zaidi msaada wa kisheria kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumbani na katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Akinukuu ripoti ya LSF yam waka 2020, N’wanakilala amesema kuwa ripoti hiyo inaonyesha kuwa takribani watu 99,844 waliweza kupatiwa huduma za msaada kisheria nchi nzima, ambapo katika yao wanawake walikuwa 60,203 sawa na asilimia 60 na wanaume 39,641 sawa na asilimia 40.
“Ripoti yetu inaonyesha katika kila matukio (4) ya ukatili yaliyoripotiwa na wanawake yalihusisha unyanyasaji wa kijinsia, ambapo visa vyote vilivyoripotiwa vinakadiriwa kufikia asilimia 26.5 kwa mwaka 2020,” amefafanua Lulu Ng’wanakilala.
Kwa miaka 10 sasa LSF chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) nchini Tanzania, imekuwa ikitekeleza programu ya upatikanaji wa haki nchini kwa kutoa ruzuku kwa mashirika zaidi ya 200 nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar ambayo yanatoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na huduma za wasaidizi wa kisheria
Katika jitihada za kuendelea kuboresha mazingira ya upatikanaji wa haki nchini Tanzania, LSF imeshasaini makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Katiba na Sheria Sheria kwa upande wa bara pamoja Wizara ya nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora kwa upande wa Visiwani.
Aidha LSF imeshasaini makubaliano na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto. Kupitia Wizara hizi, LSF imeweza pia kufanya kazi kwa karibu zaidi na Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi, Mahakama, na Magereza nchini Tanzania.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment