Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya vijana iliyopo mkoani hapa.
Wakati huo huo Wajumbe wa kamati hiyo wamewataka vijana kuchangamkia fursa ya program ya kukuza ujuzi kwa vijana inayofadhiliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwani itawakomboa kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa jana kwa nyakati tofauti na wajumbe wa kamati hiyo wakati wa ziara yao ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo ya vijana iliyopo Manispaa ya Singida.
Wajumbe hao waliwasihi vijana hao kujikita zaidi kwenye mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kujiajiri na kuondokana na dhana ya kutaka kuajiriwa.
Mafunzo wanayojifunza ni ya fani za umeme, ushonaji nguo, mapambo,useremala,ujenzi na kupaka rangi.
Miradi waliyoitembelea ni ile ya vijana waliowezeshwa na Serikali kupitia asilimia nne ya mapato ya ndani.
Awali akitoa neno la utangulizi Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Jamal Katundu alisema nia ya kamati hiyo kwenda Singida ni kutokana na kazi nzuri ya miradi walioifanya kwa asilimia 100 na kupitishwa bila ya kukataliwa kufuatia usimamizi mzuri wa vikundi vya vijana mkoani hapa.
Katika ziara hiyo wajumbe hao walipata fursa ya kuzungumza na vijana wanaopata mafunzo mbalimbali ya ufundi katika vyuo vya Veta, FDC, na SabaSaba Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu ambapo pia walitembelea miradi yote iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru na kukagua bidhaa za vijana hao kwenye Maonyesho yaliyofanyika Chuo cha Veta yaliyo andaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliokuwa kwenye ziara hiyo ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Jamal Katundu na Mwenyekiti wa kamati hiyo Najma Murtaza Giga.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment