KAMPENI YA USAJILI WA WALIPAKODI WAPYA YAWAVUTIA WENGI | Tarimo Blog



Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam

Kampeni ya usajili wa walipakodi wapya inayoendelea katika maeneo ya Ilala, Kinondoni, Kigamboni, Karikaoo, na Temeke mkoani Dar es Salaam, imewavutia wafanyabiashara wapya ambao walikuwa hawajasajiliwa katika mfumo wa kodi.

Kampeni hiyo inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni miongoni mwa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuitaka TRA kuongeza wigo wa walipakodi nchini.

Akizungumzia kampeni hiyo, Mlenzi Selemani ambaye ni msimamizi wa zoezi hilo katika Wilaya ya Temeke alisema kuwa, pamoja na maelekezo ya Rais, TRA imeamua pia kuwasogezea huduma karibu walipakodi ambapo mwitikio wake umekuwa mkubwa.

"Pamoja na kutekeleza agizo la Mhe. Rais, tumeamua kutoka kwenye ofisi zetu ili kusogeza huduma karibu na wafanyabiashara ambao wengine wanashindwa kuja ofisini kutokana na changamoto mbalimbali. Tunashukuru watu wamejitokeza na kusajiliwa kuwa walipakodi".

Selemani amewahimiza wafanyabiashara wote wapya kutembelea vituo vilivyowekwa maeneo mbalimbali hapa Dar es Salaam kwenda kupata huduma ya kusajiliwa na kupatiwa Cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

"Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara wapya kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vilivyowekwa katika maeneo ya Ilala, Kinondoni, Kigamboni, Karikaoo, na Temeke ili waweze kusajiliwa na kupatiwa TIN".

Naye mfanyabiashara kutoka Temeke, Rukia Ganya ameishukukuru TRA kwa kumuelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja na kumsajili kuwa mlipakodi.

"Ninaishukuru TRA kwa kuleta kituo cha usajili hapa Temeke, mimi ni mfanyabiashara mpya na sikujua kama natakiwa kuwa na TIN lakini maafisa wa TRA wamenielimisha na nimesajiliwa rasmi kuwa mlipakodi".

Kwa upande wake mfanyabiashara wa Tandika sokoni Manga Bakar alisema kwamba, kitendo cha TRA kuweka vituo vya usajili katika maeneo mbalimbali hapa Dar es Salaam imerahisisha kuokoa muda wa kuwafuata ofisini ambapo wakati mwingine kunakuwa na foleni kubwa ya wateja wanaotaka huduma.

Kampeni hii ya usajili wa walipakodi wapya ni endelevu ambapo kwa hapa Dar es Salaam, zoezi hili litamalizika tarehe 31 Agosti, 2021 na kuelekea katika mikoa mbalimbali nchini.

Ikumbukwe kwamba, kampeni hii ilizinduliwa rasmi tarehe 5 Agosti, 2021 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amosi Makala ikiwa na lengo la kuongeza wigo wa walipakodi na kuongeza makusanyo ya Serikali. 

Baadhi ya wafanyabiashara wapya waliojitokeza kusajiliwa katika eneo la Segerea Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam wakati wa Kampeni ya Usajili wa walipakodi wapya inayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Joseph Edward akimkabidhi Cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) Mfanyabiashara wa eneo la Tandika Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam wakati wa Kampeni ya Usajili wa walipakodi wapya inayoendelea mkoani Dar es Salaam. (PICHA NA MPIGAPICHA WETU)

Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Dinnah Lwaga akimkabidhi Cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) Mfanyabiashara wa eneo la Segerea Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam wakati wa Kampeni ya Usajili wa walipakodi wapya inayoendelea mkoani Dar es Salaam.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2