Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kumsimamia mkandarasi Proactive Independent Group anayejenga Daraja la Mbaka lenye urefu wa mita 40 kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Mhandisi Kasekenya ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Katumba – Mbambo – Tukuyu yenye urefu wa kilometa 81; sehemu ya Bujesi – Mbambo (km 11.7) na Tukuyu – Mbambo (km 7) inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza mkandarasi huyo kuongeza vifaa eneo la kazi na kuongeza muda wa kazi ili kukamilisha barabara unganishi sambamba na Daraja la Mbaka.
"Serikali tayari imekwishatoa fedha hivyo sioni sababu ya msingi Daraja hili kutokamilika kwani limekuwa linapigiwa sana kelele na wananchi wa Rungwe na Busokelo”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Naibu Waziri huyo amesema ujenzi wa daraja hilo linalohudumia wananchi wa Kyela, Tukuyu na Rungwe linajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.4 na litakuwa na barabara unganishi zenye urefu wa mita 500 kila upande ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 69.6.
Ameongeza kuwa Serikali haitamuongezea muda mwingine mkandarasi kukamilisha kazi za daraja hilo kwa mwaka ujao kwani daraja lililopo hivi sasa halina uwezo wa kubeba magari makubwa yenye uzito mkubwa na hivyo wananchi wanauhitaji mkubwa wa daraja hilo.
Aidha, Mhandisi Kasekenya ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo kutaharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya ya Rungwe na Busokelo kwani kutaboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji wa abiria pamoja na mazao yanayopatikana kama vile Kokoa, Parachichi, Tangawizi, Ndizi, Maweze, n.k
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amekagua matengenezo ya barabara kuu inayoanzia Uyole hadi Kasumulu yenye urefu wa kilometa 102.5; sehemu ya Ilima (km 3) ambapo imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kutokana na uwepo wa maji mengi ya mvua kutoka milimani na kuridhishwa na maendeleo yake.
“Nimeridhishwa na ujenzi wa kipande hiki cha kilometa tatu ambao umeanza mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza kwani mmeamua kukijenga upya kipande hiki kwa kuweka mifumo itakayoweza kupitisha maji kwa chini bila kuathiri tuta la barabara lakini pia kujenga mitaro mikubwa na kutatua tatizo la eneo hilo”, amefafanua Naibu Waziri Kasekenya.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya, Mhandisi Given Njiro, amemuahidi Naibu Waziri Kasekenya kuwasimamia wakandarasi hao wanaoendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mkoa wake kikamilifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dkt. Vincent Anney, amemshukuru Naibu Waziri Kasekenya kufika mpaka wilayani kwake na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja pamoja na barabara na kumuahidi kuendelea kusimamia kwa karibu miradi hiyo.
Mkuu wa Wilaya huyo ametoa wito kwa TANROADS kumsimamia mkandarasi huyo katika kuhakikisha ajira zinatolewa kwa wazawa wa maeneo ya mradi kwanza ili kuongeza pato la wananchi na kuilinda miundombinu hiyo.
Mbunge wa jimbo la Kyela, Mheshimiwa Ally Jumbe, ameishukuru Serikali Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara, madaraja na bandari, kwani itainua shughuli za kiuchumi katika jimbo lake na Mkoa.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment