Makamu wa Pili awataka wananchi kwenda kupata Chanjo ya Covid- 19 | Tarimo Blog

 


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali kupitia wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imetangaza vituo vya kutolea huduma za Chanjo ya Covid- 19 kwa lengo la kuwakinga wananchi wake na ugonjwa huo.

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati akiwasalimia waumini wa Masjid Muhammad uliopo Kisauni Wilaya ya Magharibi “B” mara baada ya kukamilisha Ibada ya Sala ya Ijumaa. 

Alisema huduma ya chanjo ni ya hiyari kwa anaehitaji na inatolewa bila ya malipo kwa ajili ya kurahisisha wananchi wake waweza kupata huduma hiyo kwa lengo la kujikiinga ya maradhi ya mripuko ya Covid 19.

Alieleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imeshatangaza vituo rasmi vya kutolea huduma hiyo, na kuwataka wananchi kufata taratIbu zilizowekwa ili kuweza kupata chanjo hiyo.

Alisema chanjo hiyo ni salama kwa wananchi hivyo amewaomba waumini na wananchi kwa ujumla kuachana na upotoshaji unaofanywa na watu wachache wasiokuwa na utalamu wa masuala ya Afya.

Alieleza kuwa kuna haja kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na wimbi la maradhi ya Covid -19 kuwepo nchini ambapo wananchi wengi endapo watapata maambukizi hayo watashindwa kumudu gharama ya matibabu.

Akigusia suala la kupunguza vitendo viovu, Mhe. Hemed aliwataka waumini kushikamana na maamrisho ya dini, na maelekezo ya vitabu vitukufu vya dini ili kupata radhi za Allah (SW).

Mhe. Hemed alieleza kuwa vitendo hivyo vinaondoa Baraka katika nchi, na kuwataka waumini hao kujifunza kupitia zama mbali mbali zilizopita ambazo walioangamizwa kwa kufanya matendo maovu, matendo ambayo yameshamiri katika maeneo mbali mbali Zanzibar.

Alieleza kwamba Zanzibar ilikuwa ikisifika kwa matendo mazuri, hivyo si vyema kujivika matendo maovu ambayo yanapuinguza na kushusha hadhi ya wananchi wa Zanzibar.

Akitoa khutuba Msikitini hapo Sheikh Omar Mgeni aliwataka waumin wa Dini ya Kiislamu kushikamana na Sheria za Allah, ili kujijengea mustakbali mzuri wa maisha ya Akhera.

Shekh Omar alisema kukitihiri kwa maasi katika jamii ni moja kati ya dalili za kuonesha mwisho wa dunia, na kuwanahisi waumini hao kufuata maarimsho ya Allah Mtukufu. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwakumbusha waumini na wananchi kwa ujumla kujitokeza Kupata Chanjo ya Covid – 19 Kupitia Vituo vilivyotangazwa na serikali mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa Masjid Muhamed uliopo Kisauni.

Waumini wa Masjid Muhamad Kisauni wakimskiliza kwa Makini Mhe. Hemed wakati alipopewa fursa ya kuwasalimia waumini hao mara baada ya kutekeleza Sala ya Ijuma katika Mskiti huo.




Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2