NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI ATEMBELEA DARAJA LA RUHUHU WILAYANI LUDEWA | Tarimo Blog

Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Kufuatia malalamiko yaliyotolewa hivi karibuni na wananchi wa kata ya Ruhuhu na Manda zilizopo wilayani Ludewa mkoani Njombe juu ya adha wanazozipata kwa kutokuwepo kwa daraja na kivuko imepelekea naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya kufika katika eneo la ujenzi wa daraja la Ruhuhu na kujionea uhalisia wake.

Naibu waziri huyo akiwa sambamba na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga na baadhi ya viongozi wa serikali na chama cha mapindiuzi walifika darajani hapo na Kuwasikiliza wananchi pamoja na kujionea hatua zilizofikia katika ujenzi wa daraja hilo.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kuwapokea wageni hao naibu waziri huyo amesema mbunge wao Joseph Kamonga amekuwa akilisemea bungeni daraja hilo huku akimfuata mara kwa mara kumkumbusha ukamilishwaji wa daraja hilo kitu ambacho kimemlazimu kufika katika eneo husika ili kuona uwezekano wa kumalizia daraja hilo.

"Leo nimemaliza kesi ya mbunge wenu ambayo alikuwa akinitaka mara kwa mara kuja kuona changamoto zenu za kukosa daraja na kuwaeleza mikakati ya serikali katika kumalizia ujenzi huu hivyo habari njema ni kwamba ndani ya wiki mbili zijazo vifaa vya kutandika hapa juu vitaanza kuletwa sambamba na mafundi wa kutosha ili kukamilisha hatua zilizobaki hivyo kuanzia sasa Kamonga sitarajii kama utaendelea kuwa na maswali ya nyongeza bungeni juu ya daraja hili ", alisema Mhandisi Kasekenya.

Ameongeza kuwa changamoto walizonazo wananchi hao kutokana na kukosa daraja hilo rais Samia Suluhu Hassan anazifahamu kwakuwa tayari alikwisha pita katika eneo hilo wakati wa kampeni  kipindi akiwa makamo wa rais hivyo aliahidi kutatua kero hiyo hivyo ndani ya miezi michache kero hiyo itamalizika.

Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amempongeza waziri huyo kwa kufika katika daraja hilo na kutoa tumaini jipya kwa wananchi hao kwakuwa ni matumaini yao makubwa kwamba daraja hili litakapokamilika litakuwa msaada mkubwa sana kwao.

Amewataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kipindi kifupi kwani serikali imesikia kilio chao na inaenda kumalizia daraja hilo.

" Kilio chenu wananchi wangu nimekifikisha na ndiomaana kama mnavyoona ujio huu wa naibu waziri ni hatua mojawapo ya kusikika kwa kilio chenu, uwepo wa daraja hili ni ndoto ya muda mrefu mliokuwanayo na sasa ndoto hii inaenda kutimia", Alisema Kamonga.

 Ikumbukwe kuwa siku chache zilizopita Wananchi hao walitoa malalamiko ya kukosa soko la zao la mpunga pamoja na kushindwa kupata huduma ya afya katika hospital ya Peramiho baada ya mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga kuwasili katika kijiji cha Kipingu kusikiliza changamoto za wananchi wake na kupelekea kuchukua hatua za haraka za kumleta naibu waziri huyo.

Wananchi hao walidai kuwa mwaka huu wamevuna mpunga mwingi kiasi ambacho kingewawezesha kupata  kipato kikubwa lakini  badala ya kuuuza wanaishia kuhifadhi ndani kwakuwa wanunuzi wanaowategemea  wanashindwa kuvuka kuja upande wa pili.

 Mkazi wa kijiji cha Kipingu kata ya Ruhuhu akiwa amepiga magoti mbele ya naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Godfrey Kasekenya pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuomba msaada wa kukamilishiwa ujenzi wa daraja la Ruhuhu

 

Wananchi wakiwa wameejikusanya kumsikiliza naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Godfrey Kasekenya pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kulia) akimueleza naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Godfrey Kasekenya(kushoto) juu ya changamoto wanazozipata wananchi wa kata ya Ruhuhu na Manda.

Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga wakiongea na baadhi ya wananchi wa kijiji cha kipingu kata ya Ruhuhu
Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi (kushoto) akiongea na mbunge wa jimbo la Ludewa pamoja na katibu siasa na uenezi wa wilaya ya Ludewa
Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Godfrey Kasekenya (kulia) sambamba na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga (kushoto mwenye barakoa) pamoja na Baadhi ya viongozi wa serikali wakielekea eneo la ujenzi wa daraja la Ruhuhu
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2