SERIKALI YAOKOA NDOTO ZA WASICHANA WENGI WALIOKUA WAMEACHA SHULE KWA KUANZISHA KOZI YA ELIMU HAINA MWISHO | Tarimo Blog

Mandhari na muonekano wa juu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi FDC Wilayani Rungwe Mbeya ambacho pia kinatoa kozi ya elimu haina mwisho.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi FDC Wilayani Rungwe Mbeya, Mussa Mturuki akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake waliofika kujionea uendeshaji wa Chuo hicho.
Wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi FDC Wilayani Rungwe Mbeya ambao wanasomea fani ya Ufundi umeme wa magari wakitoa maelezo ya namna wanavyoweza kutengeneza gari kwenye mifumo ya umeme.
Viongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Katumba Wilayani Rungwe Mbeya wakiwa katika picha ya pamoja na wandishi mbalimbali wa habari waliofika chuoni hapo kujionea maboresho yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.


Mmoja wa Wasichana ambao walikua wameacha shule kwa kupata ujauzito, Prisca Mwakibinga akielezea jinsi ambavyo alipata mimba na kuacha shule akiwa kidato cha tatu na Sasa anasoma kupitia kozi ya elimu haina mwisho katika Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi FDC Wilayani Rungwe, Mbeya.

 
Charles James, Michuzi TV

MABORESHO makubwa yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) yamesaidia kuanzishwa kwa kozi mpya za Elimu haina mwisho na Elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya watoto.

Akizungumza na wandishi wa habari, Mussa Mturuki ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Katumba Wilayani Rungwe, Mbeya amesema uanzishwaji wa kozi hizo umechangia kuamsha ndoto za wasichana wengi ambao walikua wamekata tamaa ya masomo.

Mpango huo wa elimu ulianzishwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu ili kumaliza changamoto ya kushindwa kupata elimu iliyokua ikiwakabili wanafunzi wa kike ambao wamekua wakiacha shule au kufukuzwa kwa sababu ya kupata ujauzito, kukosa sapoti ya mahitaji ya msingi jambo linalowapelekea wengi kuacha Shule kwa kuona ni mzigo.

Kupitia mradi huu wa Elimu haina mwisho wanafunzi hawa wanapata elimu ya Sekondari kwa kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kwa miaka miwili huku pia wakipewa fursa ya kuchagua fani mojawapo ya kusoma katika kipindi hicho.

" Kwa kweli tunashukuru Serikali kwa kufanya maboresho kwenye Vyuo hivi kwani vimesaidia hizi kozi kuanza na zimekua na matokeo chanya sana kwa watoto hawa, kwa sababu licha ya kupata fursa ya kumaliza masomo yao ya sekondari lakini pia hupata fursa ya kuchagua kozi ya fani mojawapo ikiwemo upishi, ufundi ujenzi, umeme wa magari, ufundi seremala n.k.

Mpaka sasa tuna wanafunzi 30 wa elimu haina mwisho ambapo pia wanapata fursa ya watoto wao pia kusoma na kulewa kwenye vituo hivi vya serikali vinavyotoa elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto," Amesema Mturuki.

Amesema katika Chuo chao hicho cha Katumba wana idadi ya watoto 90 ambao wanalelewa katika kituo hiko cha watoto ambavyo vimekua vikijulikana kwa jina la Day Care.

Akizungumzia ukarabati uliofanyika chuoni hapo, Mturuki amesema Chuo chao kilipokea kiasi cha Milioni 606 kwa ajili ya maboresho ambapo walitumia fedha hizo kujenga majengo mapya na kukarabati ya zamani.

"Kipekee tuishukuru sana Wizara ya Elimu kwani baada ya Vyuo hivi kuwekwa chini ya Wizara hii Mwaka 2017 hapo hapo walianza kazi ya kutuboreshea miundombinu yetu kwenye Vyuo vyote 54 nchini.

Sisi hapa Katumba tuliletewa Sh Milioni 606 ambayo tulitumia kujenga majengo mapya ikiwemo bweni la kisasa lenye kubeba wanafunzi 100, ujenzi wa Karakana ya Umeme, ushonaji na magari na ukarabati wa majengo ya zamani sita likiwemo jengo la Utawala, bweni la kiume, ukumbi, bwalo na jiko pamoja na madarasa mawili," Amesema Mturuki.

Amesema uwepo wa kozi hiyo umekua msaada mkubwa wa Wasichana ambao walishakata tamaa huku akisisitiza kuwa hakuna gharama zozote ambazo wanafunzi hao hulipa kwani Wizara huhudumia kila kitu.

Nao wanafunzi wanaonufaika na mradi huo wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuanzisha kozi hizo ambazo hazikuepo awali mwenye Vyuo vya FDC kwani vimeamsha matumaini ya kutimiza ndoto zao ambazo zilikua tayari zimeshakufa.

" Ni wazi sikua na matumaini tena ya kusoma baada ya kupata ujauzito, shuleni nilifukuzwa na nyumbani niilitengwa, lakini baada ya kusikia tangazo la Chuo hiki kanisani kwetu sikusita kuchukua fomu na kujaza, hivi sasa nakaribia kumaliza elimu yangu ya kidato cha nne na nina matarajio ya kusonga mbele zaidi.

Faida nyingine tunayoipata sisi ambao tuna Watoto ni kwamba tunakuja na Watoto wetu ambao nao wanalelewa kwenye hii Day Care iliyopo hapa, tunaishukuru sana Serikali kupitia Wizara yetu ya Elimu," Amesema mmoja wa wanafunzi hao Prisca Mwakibinga.

Nae Sada Amani ameishukuru Serikali kwa kufufua ndoto zao hasa baada ya kukaa nyumbani muda mrefu ambapo ameahidi kufanya vizuri kwenye masomo yake na kusonga mbele zaidi katika kukimbilia ndoto alizonazo.

" Tunaishukuru sana Serikali wengi wetu tulishapoteza matumaini kabisa lakini wao wametufuta machozi na sasa tunatimiza ndoto zetu, ahadi yetu kwao ni moja tu kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zetu za kuja kujiinua kiuchumi sisi binafsi na Taifa letu kwa ujumla.

 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2