CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo,(CHADEMA), kubadilika na kuanza kufanya siasa za hoja, zenye kutoa kipaumbele maendeleo ya wananchi na Taifa badala ya siasa za kuhimiza ghasia, vurugu na kueneza uongo na chuki nchini.
Pia chama hicho kimemtaka Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika kuacha upotoshaji na kumlisha maneno Rais Samia Suluhu Hassan ambayo hakuyasema au kuingilia mwenendo wa kesi ya Mbowe mahakamani .
Hayo yameelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka alipoulizwa kuhusu tuhuma alizozitoa Mnyika alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari.
Amesema katika maelezo ya Rais Samia aliyoyatoa wakati wa mahojiano na. Shirika la Utangazaji Uingereza(BBC Swahili yaliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam amesema hakuna mahali demokrasia imeminywa nchini na ndio maana vikao vya kikatiba vya vyama mbalimbali vya siasa nchini vinaendelea.
Aidha alisisitiza siasa zenye mrengo wa vurugu na ghasia hizo hazina nafasi na wala hazitavumiliwa kwani hiyo sio demokrasia. Hivyo Mnyika aache kumlisha maneno Rais Samia.
Kuhusu sakata la kesi ya Mwenyekiti wa Chadema inayoendelea Mahakama ya Kisutu hakuna pahala katika maelezo yake Rais Samia wakati wote wa mahojiano aliingilia uhuru wa mahakama kama Mnyika alivyopotosha zaidi alitaka watu kuwa watulivu waipe nafasi mahakama kutekeleza wajibu wake.
"Chadema waache vioja vya kudai demokrasia imeminywa na hawaruhusiwi kufanya mikutano wala vikao wakati wameendesha operesheni haki, chadema kidigitali na vikao mbalimbali vya ndani bila bugudha yoyote. Lakini cha ajabu tena (leo) Mnyika ameendelea kuuingilia uhuru wa mahakama jambo ambalo linaoonyesha jinsi alivyo na papara na jazba Mnyika zinazvyomzidisha hofu kadri anavyolalamika." amesema Shaka
Amesema ni muhimu wakafahamu ikiwa maandalizi yao ya mikutano au vikao na operesheni zozote za kisiasa yatakuwa na viashiria au dhamira ya kupanga, kuratibu, kuasisi au kutekeleza vurugu na ghasia nchini vyombo vya dola havitakaa kimya sio kwao tu bali kwa yeyote yule.
Aidha Shaka amesema Rais Samia ameapa kuilinda na kuitetea Katiba ikiwemo kuhakikisha ustawi wa amani na utulivu nchini.Hivyo haitatokea hata mara moja akakubali watu wachache kwa maslahi yao wakavuruga nchi.
"Jambo jingine watanzania wanapaswa kujua Chadema sio chama kikuu cha upinzani wakati huu kwani kina mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa hivyo hawana sifa hiyo,"amesema na kuongeza ameshangazwa na dhamira ya Chama hicho kutaka kuonana na Rais wao kama wao ili hali wao sio chama pekee cha upinzani nchini.
Shaka ametoa rai kwa watanzania na wadau wote wa maendeleo ndani na Nje ya Nchi kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kwa pamoja tuifikishe Tanzania katika maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine CCM kimekanusha na kulaani vikali matamshi yaliotamkwa na viongozi wawili wa juu wa ACT Wazalendo kuhusu kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa CCM jimbo la Konde Sheha Mpemba Faki si kweli kama ni ushauri uliotolewa na Kamati Kuu ya CCM bali ni sababu za kifamilia kama barua yake aliyoiwasilisha kwenye Chama chake ilivyoeleza.
Pia kimemtaka Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho Juma Duni Haji na Mjumbe wa Kamati kuu ya chama hicho Othman Masoud Othman kuacha siasa za udanganyifu na upotoshaji na kuhakikisha wanamudu siasa za hoja.
Akizungumza zaidi, Shaka Hamdu Shaka amesema CCM kimeshangazwa na matamshi ya viongozi hao kuzungumza maneno ya kuwapotosha wafuasi wao na kuwadharau kwa kuwaeleza uongo wakidai walikutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kuzungumzia uchaguzi wa jimbo la Konde.
Shaka amesema hakuna kikao chochote walichowahi kukaa na Rais Samia popote sio tu kwenye ardhi ya Tanzania hivyo waache uzushi." Viongozi hao wanapaswa kuacha siasa za mazoea, unafiki, na uzandiki kwa kudanganya wanachama ambao wamekuwa wakihama nao kila wanakokwenda mambo mbalimbali."
Amefafanua tabia waliyokuwa nayo tokea mwaka 1995 wakiwaburuza kifikra wafuasi wao na kuwaahidi wangepewa madaraka ya kuitawala Zanzibar na mataifa ya Nje kila siku bila ahadi hiyo kutimia huku wakisahau ridhaa ya kuiongoza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatolewa na wazanzibar wenyewe.
Aidha amesema Kamati Kuu ya CCM haiwezi kuitishwa ghafla kwa ajili ya kujadili agenda yoyote inayokihusu Chama cha ACT-Wazalendo aidha kwa migogoro yake ya ndani, kususia kwake kushiriki au kutoshiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kwani huko nyuma wakiwa CUF waliwahi kususa na mambo yakaendelea, hivyo amemtaka Duni na mshirika wake waache propaganda.
Shaka amekitaka ACT Wazalendo na viongozi wake kuacha sarakasi zake na mazoea ya siasa zinazoambatana na propaganda ikiwemo kuidanganya dunia badala yake kiwe chama chenye siasa za kweli, zenye uzalendo na kupigania mabadiliko ya ustawi wa maisha ya wananchi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment