TAASISI ya Wajibu imeandaa mkutano wa wadau wa fani tofauti tofauti ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo uwazi wa kifedha na uwajibikaji kama nyenzo kwa nchi za Afrika kufikia maendeleo endelevu ya ushindani katika uchumi wa dunia.
Akizungumzia mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU, Ludovick Utouh amesema kwamba wanatarajia mkutano huo utahusisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali zikiwemo taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, wanadiplomasia, wanaazaki, wabobezi wa masuala ya uwazi na uwajibikaji, wanataaluma mbalimbali pamoja na wanahabari kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema mada nyingine ambazo zitatolewa ni uhuru wa ofisi za ukaguzi za nchi na athari zake kwenye uwazi na uwajibikaji katika mabadiliko kwenye kanuni na mazoea ya ufanyaji ukaguzi wa ndani na nje.
" Je! Serikali za Afrika zina uwazi na uwajibikaji wa kutosha katika kushughulikia janga la covid – 19?Ufanisi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kuimarisha Uwazi na uwajibikaji wa Fedha na Rasilimali za Umma barani Afrika," Amesema Utouh.
Amesema kuwa itatolewa pia mada ya kuwa wazi zaidi na kuwajibika na mipango ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika sekta ya uziduaji barani Afrika.
Utouh amesema uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa Serikali zote duniani una umuhimu wa kipekee katika kuletea wananchi maendeleo.
" Ninatoa rai kwa wadau wote wa uwazi na uwajibikaji kutoka ndani na nje ya nchi kuweza kushiriki Mkutano huu wa Kimataifa wa ITAC 2021 ambao ni fursa ya kujadili na kubadilishana mawazo ya nini kifanyike ili kukuza na kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa maendeleo ya nchi za Afrika.
Tunatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 500 wa mkutano huo. Vilevile, wanatarajia kuwa na Mgeni rasmi ambaye ni mmoja wa viongozi wakubwa kitaifa nchini, ila kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu hatuwezi kumtaja hivi sasa," Amesema Utouh.
Mkutano huo unatarajia kufanyika Novemba 18-19 mwaka huu katika Hotel ya Mount Meru iliyopo jijini Arusha.
Kwa habari na Maelezo zaidi bofya https://www.wajibu.or.tz/
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU, Ludovick Utouh (wa pilia kushoto) akiwa na baadhi ya Wadau wengine wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji ( International Transparency and Accountability Conference – ITAC) unaotarajiwa kufanyika kwa siku mbili, kuanzia tarehe 18 hadi 19 Novemba, 2021 katika Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha, Tanzania
wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji ( International Transparency and Accountability Conference – ITAC),pia kulikuwepo na majadilialiano ya mada kutoka kwa Wadau zilizohusu mambo ya uwazi na uwajibikaji
Meneja wa Utafiti na Miradi kutoka Taasisi ya WAJIBU, Moses Kimaro akiwakaribisha Wadau mbalimbali waliofika kushiriki maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji ( International Transparency and Accountability Conference – ITAC) unaotarajiwa kufanyika kwa siku mbili, kuanzia tarehe 18 hadi 19 Novemba, 2021 katika Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha, Tanzania
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU, Ludovick Utouh (katikati) akiwa na baadhi ya Wadau wengine wakifuatilia mada zilizokuwa zikijadiliwa mara baada ya uzinduzi wa maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji ( International Transparency and Accountability Conference – ITAC) unaotarajiwa kufanyika kwa siku mbili, kuanzia tarehe 18 hadi 19 Novemba, 2021 katika Hoteli ya Mount Meru, Jijini Arusha, Tanzania.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment